Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilianza mpango wa CHF iliyoboreshwa mnamo mwezi Februari mwaka 2019 ambapo hadi sasa zaidi ya wananchi 7018 sawa na kaya 1275 wameshajiandikisha kunufaika na huduma hii tangu kuanza kwa mpango huu.
Adventina Masululi ni mratibu wa bima ya afya iliyoboreshwa ya CHF katika Manispaa ya Ilemela amesema kuwa, bima hii inatoa fursa kwa mtu mmoja hadi sita katika kaya kujinga na kulipia gharama ya kiasi cha shilingi za kitanzania 30,000 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa, mwananchi yoyote ambae hana kadi ya bima ya afya anaruhusiwa kujiunga na bima hii iliyoboreshwa ambapo mwananchi atafika katika mtaa husika na kujiandikisha kwa ajili ya kujiunga na mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote atapatiwa kadi papo hapo.
Aidha aliendelea kufafanua faida ya kuwa mwanachama wa bima hii ikiwemo kupata huduma za afya katika vituo vyote vya Serikali bila ya kuwa na fedha taslimu, kupata huduma kwa gharama nafuu ukilinganisha na idadi kubwa ya namba ya watu wanaonufaika.
‘.. Bima hii ya afya iliyoboreshwa itamsaidia mwananchi kupata huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali kwa gharama nafuu na kwa haraka ...’ Alisema
Pamoja na hayo alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo katika mpango wa Bima ya afya iliyoboreshwa ikiwemo upungufu wa vifaa vya kutendea kazi, baadhi ya maafisa waandikishaji kutowasilisha kwa wakati michango inayotolewa na wanufaika na ugeni wa teknolojia inayotumika katika kufanikisha zoezi hilo.
Mwanafunzi Amina Hasani na Bi Mwanne German ni miongoni mwa wanufaika wa bima ya afya iliyoboreshwa ya CHF Kutoka kata ya Nyakato, manispaa ya Ilemela ambapo wametaja manufaa waliyoyapata kwa kuwa wanachama wa huduma hiyo zikiwemo kupata huduma kwa haraka na gharama nafuu huku wakiamini kuwa bila uwepo wa huduma hii ingekuwa ngumu kwa wao kugharamia matibabu kutokana na hali ya uchumi waliyonayo.
CHF iliyoboreshwa ni bima ya afya ya jamii ambayo ina lengo la kusaidia jamii ya Kitanzania kupata huduma ya matibabu ya afya kwa gharama nafuu, kwa kupata matibabu ya afya kwa mwaka mzima kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya na mkoa kwa rufaa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.