Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI chini ya mradi wa EP4R leo tarehe 5 Agosti, 2025 Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imepokea vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na viti mwendo, mafuta maalum na kofia za kujikinga na jua kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi, visaidizi vya usikivu hafifu na vinginevyo mbalimbali.
Akipokea vifaa hivyo afisa elimu msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mwl. Mashelo Bahame ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwani vifaa hivyo vitawezesha wanafunzi kuweza kusoma vizuri bila changamoto na kufaulu mitihani yao.
“Nakiri kupokea vifaa mbalimbali vya watoto wenye mahitaji maalum kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ambavyo vinatokana na mradi wa EP4R na tayari tumeshavisambaza kwenye shule zetu kama maelekezo yalivyotolewa na viongozi pia nitoe rai kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalum kutowaficha watoto hao badala yake wawapeleke shule kwa ajili ya kujifunza stadi mbalimbali” alisema afisa elimu huyo", amesema Mwalimu Mashelo
Naye Mwl. Ibrahim Mtigandi, mwalimu kutoka shule ya sekondari ya wavulana Bwiru kwa niaba ya walimu wanaofundisha kwenye shule zenye watoto wenye mahitaji maalum ameishukuru serikali kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuwaletea vifaa saidizi kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule zao.
“Vifaa hivi vitawasaidia wanafunzi wetu kujifunza na kukuza uelewa na pia kwetu sisi walimu vitataturahisishia kufundisha kwa vitendo ” alimaliza Mwl. Mtigandi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.