" Napenda kusisitiza kuwa upandaji wa miche ya matunda uwe endelevu,sambamba na utoaji wa elimu ya lishe kwa vitendo (shamba darasa), pelekeni huduma hii katika shule na zahanati nyingi zaidi ili watoto wetu na jamii kwa ujumla waendelee kujifunza elimu ya lishe kwa vitendo"

Rai hii imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe. Amiri Mkalipa Tarehe 20/11/2025 katika maadhimisho ya siku ya kitaifa yaliyofanyika katika mtaa wa Imalang’ombe kata ya Sangabuye huku akibainisha dhumuni la maadhimisho hayo kuwa ni kuongeza uelewa katika jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa jamii.
Aidha Mhe Mkalipa amewaagiza wataalamu wa lishe wilayani Ilemela kuweka mkazo zaidi kwenye kutoa elimu ya lishe katika maeneo yote ya Ilemela ili kuweza kuwa na watoto wenye afya bora kwani kufanya hivi kutasaidia kuondokana na maradhi yatokanayo na ukosefu wa lishe bora.
Sambamba na maelekezo hayo Mhe. Mkalipa pia ametoa wito kwa kina baba kutimiza wajibu wao katika malezi ya watoto kwani kuna maradhi kama vile udumavu na utapiamlo wakati mwingine husababishwa na wazazi kutokutimiza wajibu wao.
Kwa upande wake Bi. Ummy Wayayu, mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, amesema kuwa kufuatia elimu ya masuala mbalimbali ya lishe na afya iliyotolewa katika maadhimisho hayo anaamini kuwa jamii itakwenda kuyafanyia kazi kikamilifu na itakwenda kubadilika katika mtazamo chanya.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli na afua za lishe katika Manispaa ya Ilemela, Afisa Lishe Bi. Pili Kasim amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa hali ya utapiamlo kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 2.0 na pia halmashauri imefanikiwa kuanzisha kilimo cha mazao kwenye shule za msingi na sekondari 22, bustani 17 za mbogamboga pamoja na vituo vitatu vinavyotoa huduma za afya lengo ikiwa ni kuwasaidia wanafunzi na jamii kujifunza kwa vitendo elimu ya lishe.
“Nitoe wito kwa jamii kuhakikisha inafuata mtindo bora wa maisha pamoja na kuzingatia ulaji unaofaa ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.” Alisema Bi. Pili
Akizungumza Ndg. Jeremia Samweli Daniel mkazi wa mtaa wa Imalang’ombe amewaasa wazazi na walezi kuwahudumia watoto wao na kuwapatia huduma ya lishe bora ili wakue katika hali nzuri. Huku Bi. Semeni Peter mkazi wa mtaa wa Imalang’ombe ameishukuru serikali kwa kuwapelekea maadhimisho hayo na kutoa wito kwa kina baba na kina mama kushiriki kikamilifu katika matukio kama hayo.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo,"Afya ni mtaji wako;Zinagtia unachokula" yameenda sambamba na utoaji wa huduma za utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto chini ya miaka 5, upimaji wa HIV, homa ya Ini, Saratani ya matiti, huduma za macho, masikio na kinywa pamoja na shughuli mbalimbali za utoaji wa elimu ya lishe,ulaji unaofaa kwa mama mjamzito na mama anayenyonyesha, umuhimu wa kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubisho, jiko darasa, ugawaji wa unga wa lishe sambamba na upandaji wa miti ya matunda.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.