Sote tunatambua kuwa maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto kwakuwa ni salama, safi na yenye kingamwili zote ambazo zinasaidia kulinda mtoto dhidi ya magonjwa mengi ya utotoni, kujenga akili ya mtoto na kumfanya kuwa na afya njema.
Kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti (tarehe 1 mpaka 7) duniani kote huadhimisha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama ambayo hutumika kama kipindi cha kutambua unyonyeshaji wa maziwa ya mama kuwa ni msingi madhubuti wa afya bora, maendeleo na usawa katika maisha ya mwanadamu
Katika kuadhimisha wiki hii ya unyonyeshaji manispaa ya Ilemela kupitia kitengo cha Lishe, imeendelea kutoa elimu kwa wakina mama wanaonyonyesha na wajawazito na huduma hii imekuwa ikitolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na ngazi ya jamii
Akitoa elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama katika zahanati ya pasiansi leo tarehe 06 Agosti, 2025 Bi. Pilli Khasim afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela amewahimiza wakina mama wanaonyonyesha kuzingatia taratibu sahihi za unyonyeshaji ili kumjengea mtoto afya bora kimwili na kiakili.
“Mnyonyeshe mtoto ziwa moja kwa muda wa dakika 15 hadi ishirini kabla ya kumhamishia ziwa jingine hii itamsaidia mtoto asivute hewa tupu itakayomsababishia mtoto kupata shida ya gesi tumboni” alielimisha Bi. Pilli
Naye mtoa huduma ya mama na mtoto katika zahanati ya Pasiansi Bi. Savelina Kyesha amewataka kinamama kuzingatia na kuyafanyia maelekezo yaliyotolewa na wataalam kuhusiana na unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Naomi Hamisi mkazi wa mtaa wa sabasaba yeye kwa niaba ya akina mama amewashukuru wataalam kwa elimu ambayo wamekuwa wakipatiwa kwani imewasaidia kufahamu namna sahihi ya unyonyeshaji.
“Elimu tuliyopatiwa leo ni nzuri, imetusaidia kufahamu namna sahihi ya kunyonyesha, tunatarajia afya za watoto wetu zitaimarika” alisema Naomi
Kauli mbiu ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama mwaka 2025 ni “Thamini unyonyeshaji, weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto”.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.