Wavuvi katika Manispaa Ya Ilemela kupitia Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) wanatarajiia kupata manufaa makubwa mara baada ya kuzinduliwa kwa akaunti ya wavuvi kupitia bank ya Posta Tanzania.
Manufaa mbalimbali yatakayopatikana kwa wavuvi kupitia akaunti hiyo ni pamoja na kuweza kujiwekea Akiba kwa masharti nafuu kupitia TPB bank Kupata Elimu ya kifedha kupitia wataalam wa benki ya TPB, Shughuli zao zitaweza kurasimishwa na kuweza kuwa na sifa za kupata mikopo kupitia bank hiyo. Pamoja na kuchochea maendeleo ya shuguli za uvuvi katika mzunguko mzima ya uvuvi kwa maana ya wamiliki, wachakataji, mama lishe, wajeshi na wachuuzi wadogo wadogo wa samaki.
Benki ya Posta Tanzania (TPB) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) zimeingia mkataba pamoja na kutiliana saini uzinduzi wa akaunti ya wavuvi ambayo itajulikana kwa jina la Wavuvi account.
Zoezi hilo la utiaji saini limeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega katika mwalo wa Igombe uliopo Wilaya ya Ilemela ambapo amewataka wadau hao kuhakikisha wanajiunga na akaunti hiyo ili waweze kupata huduma za kifedha zitakazowawezesha zana za kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi ambazo zitawafanya kupata malighafi kwa wingi, huku akiupongeza uongozi wa TPB bank kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wavuvi katika kuwaletea maendeleo.
“Niwaombe wavuvi mfungue Wavuvi Akaunti katika Benki ya Posta Tanzania (TPB) itakuwa rahisi kwenu kupata msaada ili muweze kufanya biashara ambapo viwanda sasa vimeanza kufufuliwa upya, nasi tumeagiza kwa sasa samaki wote wanaozalishwa katika viwanda vyetu ni lazima wasafirishwe moja kwa moja kwenda nchi za nje kupitia viwanja vyetu vya ndege badala ya kusafirishwa kwenda nchi zingine kupitia viwanja vya ndege vya nchi jirani.” Amesema Mhe. Ulega
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) Bw. Sabasaba Moshingi alisema utiaji saini kati ya benki hiyo na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA), ni muhimu kwa kuwa huduma ya Wavuvi Akaunti itawawezsha wavuvi wengi kuwa na utaratibu wa kutumia huduma za kibenki kwa kuwa kwa sasa wengi wao utumiaji wao wa huduma za kibenki upo chini.
Naye Katibu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) Bw. Bakari Kadabi aliwaomba wananchi wote kuungana kutokomeza uvuvi haramu na kuuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuongeza mnyororo wa thamani kwa wavuvi na vikundi kujiunga na chama kikuu ambapo mkataba huo na TPB utawawezesha wadau wa sekta ya uvuvi kupata elimu ya fedha na kukopeshwa na benki hiyo kwa ajili ya uendelezaji wa kazi zao.
Zoezi hilo la utiaji saini lilifanyika siku ya tarehe 23.09.2019 huku likishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ilemela akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na wananchi mbalimbali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.