"Hatutarajii tusikie mafunzo yetu yametumika vibaya miongoni mwenu, kwa kutumia kiapo kile hatutakuacha salama , tutakushughulikia kwa mujibu wa sheria”
Kauli hiyo imetolewa na Mhe Amir Mkalipa, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela akifunga mafunzo ya awali ya jeshi la akiba wilaya ya Ilemela kwa askari 121 wa Jeshi la Akiba, wakiwemo wanaume 101 na wanawake 20 siku ya Jumanne ya tarehe 09 Septemba 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Lumala.
Aidha Mhe. Mkalipa amewapongeza wahitimu kwa nidhamu na juhudi walizoonyesha wakati wote wa mafunzo na pia amewahimiza kuwa mabalozi wa amani, uzalendo na wawe watetezi wa wanyonge katika jamii wanakotoka.
Naye Mshauri wa mgambo wa wilaya ya Ilemela Meja Ramadhan Mbego amesema wahitimu wamepata mafunzo mbalimbali ambayo yamewajengea ujasiri na utayari wa kukabiliana na adui, uzalendo pamoja na kulitumikia taifa.
"Tumewapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ukakamavu, ujanja porini, kusoma ramani, kutumia silaha, mbinu za kivita, mafunzo ya utimamu wa akili pamoja na elimu ya uraia hivyo tunaamini wameiva na wako tayari kulitumikia taifa" alisema Meja Mbego
Akisoma risala mbele ya Afande Mgeni rasmi kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, Mg. Elizaberth Gabriel Mabula ameiomba serikali kuwatazama kwa jicho la tatu na kuwapa kipaumbele katika fursa za kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa miezi minne yamehitimishwa kwa askari hao kuapa kiapo cha utii kikiambatana na sherehe za gwaride, kareti pamoja na kikosi cha singe huku Afande mgeni rasmi akiwatunuku vyeti Askari walioonesha umahiri katika medani mbali mbali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.