Wajumbe 135 wa mabaraza ya Kata 19 za Manispaa ya Ilemela walioapishwa wametakiwa kutenda haki pamoja na kuwasaidia wananchi kupata haki zao katika migogoro itakayojitokeza amesema Mhe. Hakimu Amani Nelson Sumari alipomaliza kuwaapisha wajumbe hao.
Hakimu Sumari, ambae ni Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, amewataka wajumbe hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufasaha na kuwa ambae hatatekeleza atachukuliwa hatua za kisheria na kuwajibishwa kwani kitendo cha kula kiapo ni wazi kuwa wamejifunga na sheria.
“Hakikisha unatenda haki, unasikiliza mashauri, na unatoa maamuzi bila ya upendeleo”, Alisisitiza
John Paul Wanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, nae amewapongeza wajumbe hao kwa kuaminiwa na kuteuliwa kutoka katika kata zao, na kuwasisitiza kuwa lengo kubwa la kazi yao ni usuluhishi wa migogoro mbalimbali inayowakumba watu katika kata zao ili kuweza kudumisha amani na utulivu ili kuweza kuleta maendeleo.
Pamoja na hayo amesisitiza kuhusu suala la viwango vya tozo na kuwaeleza kuwa kila faini au gharama ambayo mwananchi analipa anatakiwa alipe kwa mfumo wa kielektroniki na kwa mujibu wa sheria ya fedha ili kuondoa suala la rushwa na kuwa kwa kiongozi atakaekiuka taratibu hizo atachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha aliwafafanulia baadhi ya majukumu yao ambayo baadhi yake ikiwa ni kuwa hawana mamlaka ya kusikiliza migogoro ya ardhi iliyopimwa na kama watafanya hivyo watakuwa wamekiuka sheria na maamuzi hayo yatakuwa batili.
Mkurugenzi aliwasisitizia kuhusu suala la kutokuwa na upendeleo wakati wanasikiliza migogoro mbalimbali. “ Tusiamue migogoro kwa upendeleo”, alisisitiza
Nae Mstahiki Meya Mh: Renatus Mulunga aliwasisitiza wajumbe hao kuhusu suala zima la kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa wananchi pamoja na kuepukana na vitendo vya rushwa kwani hakuna mtu ambae yuko juu ya sheria, alisema.
Vilevile Afisa Mipangomiji na ardhi wa Manispaa ya Ilemela, Ndugu Shukurani Kyando nae alipata wasaa wa kuongea na wajumbe hao walioapishwa na kusema kuwa migogoro mingi katika Halmashauri inahusiana na masuala ya ardhi hivyo aliwaelekeza kuwa wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na sio kwa kufuata maono yao binafsi na kuhakikisha kuwa shauri wanalosikiliza hawana maslahi nayo.
Ndugu Ivan Masao ambae ni Mwenyekiti wa Baraza la ardhi na Nyumba Mwanza aliwapongeza Ilemela kwa kutokuwa na migogoro mingi, aidha aliwaelekeza wajumbe wa mabaraza hayo kuzingatia suala la uwiano wa kijinsia katika kusikiliza migogoro mbalimbali.
Akihitimisha zoezi hilo Mwanasheria wa Manispaa ya Ilemela, Patrick Muhere, aliwahimiza wajumbe hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ueledi na kwa kuzingatia maadili na miongozo mahsusi ili kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kurudisha imani kwa wananchi tunaowahudumiwa na haki itaoneka kutendeka katika jamii.
Mabaraza ya kata ni vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985, ambapo kila baraza linajumuisha wajumbe wasiopungua wanne na wasiopungua wanane watakaochaguliwa na kamati ya kata kutoka miongoni mwa majina ya wakazi wa kata yaliorodheshwa kwa kuzingatia taratibu maalum uliowekwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.