Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Ilemela kuyatumia mafunzo waliyopatiwa kuleta tija katika maeneo yao
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani wa Manispaa ya Ilemela ambayo yalilenga kuwawezesha madiwani hao kusimamia utendaji kazi katika utoaji huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya sheria, uongozi na utawala bora.
“Niwashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa ushiriki wenu, na kimsingi kile ambacho mmejifunza ninaamini kitaenda kuleta tija katika maeneo yenu”, Amesema Masala
Ameongeza kusema kuwa ana matumaini kuwa mafunzo waliyoyapata yatawawezesha kutekeleza majukumu yao vyema na kuwa migongano na misuguano haitakuwepo tena huku wakiendelea kuisimamia halmashauri kwa kufuata misingi ya sheria.
Oscar Tandula akimwakilisha Afisa wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Mwanza, amewapongeza madiwani kwa kujengewa uwezo na kuwahimiza masuala mbalimbali ikiwamo suala la usimamizi wa mapato kuwa ni jukumu lao ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kuchangia na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pamoja na hilo ndugu Oscar amewahimiza madiwani kuhakikisha wanapitia taarifa mkaguzi wa ndani za kila robo pamoja na kuhakikisha kuwa asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu inatumika ipasavyo na kuleta tija.
Mhe Sarah Ng’hwani wa kata ya Buswelu, kwa niaba ya madiwani wote amesema kuwa wameiva na kuwa watafuata waliyofundishwa huku akiushukuru uongozi wa Manispaa ya Ilemela pamoja na wakufunzi kutoka chuo cha serikali za mitaa cha hombolo kwa kuhakikisha kuwa madiwani wanapatiwa mafunzo haya ambayo yamekuwa ya manufaa makubwa sana kwao huku akiwahimiza waheshimiwa madiwani wenzake kwenda kuyatumia mafunzo hayo kuleta tija kwa manufaa ya wananchi na halmashauri.
Mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo masuala ya uongozi na utawala bora, uendeshaji wa vikao na mikutano katika mamlaka za serikali za mitaa, usimamizi na udhibiti wa fedha katika mamlaka za serikali za mitaa, usimamizi wa manunuzi na mikataba, usimaizi wa miradi ya kimkakati na ile ya maendeleo, usimamizi wa watumishi katika mamlaka za serikali za mitaa, maadili ya madiwani, mfumo wa ujifunzaji kielektroniki, haki na stahiki za madiwani.
Mafunzo hayo ya siku tano kuanzia tarehe 06/09/2021 hadi tarehe 10/09/2021 yaliyotolewa na wakufunzi kutoka chuo cha serikali za mitaa Hombolo, yametimishwa kwa waheshimiwa madiwani kupatiwa vyeti vya ushiriki kutoka chuo hicho.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.