Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imepongezwa kwa jinsi inavyozingatia matakwa ya Sera ya kuhakikisha inatenga na kutoa mikopo ya asilimia 4 kwa vijana, asilimia 4 kwa wanawake na asilimia 2 kwa walemavu.
Pongezi hizo zimetolewa na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ally wakati akikagua shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na kikundi cha Vijana Igombe ikiwa ni muendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya ya Ilemela
Mkongea ameisifu na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kuona umuhimu wa kutekeleza Sera hiyo ya Serikali inayosaidia vijana kupata mtaji na kujiajiri katika utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo badala ya kujikita katika mambo yasiyofaa ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya kihalifu
‘.. Nitumie nafasi hii kuipongeza halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu maana zipo halmashauri nchini hazitengi na zile zinazotenga zinatoza riba kitu ambacho ni kinyume na maagizo ya Serikali…’ Alisema
Akimkaribisha kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mheshimiwa Daktari Severine Lalika amemhakikishia kiongozi huyo kuwa wilaya ya Ilemela itaendelea kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na wananchi sanjari na kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na Serikali.
Nae Mbunge wa jimbo la Ilemela mheshimiwa Daktari Angeline Mabula amemuomba kiongozi huyo kufikisha salamu za shukrani na pongezi kutoka kwa wananchi wa jimbo la Ilemela kwenda kwa mheshimiwa Rais Daktari John Magufuli kufuatia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya jimbo hilo.
Aidha Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019,Ali Mkongea amekemea halmashauri zinazotoza riba katika utoaji wa mikopo hiyo huku akiwaasa vijana kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zinazotolewa kwa kuhakikisha wanazitumia kwa shughuli za uzalishaji mali zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi.
Hadi sasa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeshatoa kiasi cha fedha Shilingi za Kitanzania Milioni 244 kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.