ILEMELA YAPATA VIONGOZI WA JUKWAA LA WADAU WA UKIMWI
Halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaojihusisha na mapambano ya kudhibiti Ukimwi ndani ya wilaya hiyo imekutana na kuunda jukwaa la wadau wa Ukimwi ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha lengo la Dunia linafikiwa kuwa, ifikapo mwaka 2020 kutokuwepo maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza na wadau hao Mwenyekiti wa Kamati ya kudhibiti Ukimwi na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela Mheshimiwa Shabani Ramadhan Maganga amesema lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wanaopatikana ndani ya wilaya ya Ilemela katika kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Ukimwi sambamba na kuhakikisha lengo la Dunia linafikiwa la kuzuia maambukizi mapya ifikapo mwaka 2020.
“Tamaa yangu ni kuona Jukwaa hili linakuwa la mfano Ilemela na nchi nzima katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuwakutanisha wadau pamoja kujadili changamoto, kubadilishana uzoefu, kuunganishi nguvu ya pamoja ili kuifikia ile Tisini, Tisini, Tisini na lengo la Dunia la kuzuia maambukizi mapya ifikapo mwaka 2020 na hili linawezekana tushirikiane katika kusimamia jambo hili”, Alisisitiza.
Pamoja na hayo wadau hao walifanya uchaguzi wa viongozi wake ikiwa ni hatua za awali kabla ya uzinduzi ambapo Ndugu Joseph Bukura alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Ndugu Msumari alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti, wakati Bi Edina Edward alichaguliwa kuwa katibu na Bi Joyce Benjamini kuwa Muhazini wa Jukwaa.Uongozi huo utakuwa ni wa kipindi cha mwaka mmoja.
Nao wadau walioshiriki katika mchakato wa uundaji Jukwaa hilo mbali na kuishukuru Manispaa ya Ilemela chini ya Naibu Meya wake Mhe Shaban Maganga kwa uamuzi wake wa kuona haja ya uwepo wa Jukwaa hilo wameahidi kuhakikisha wanalitumia vyema Jukwaa hilo katika kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi sanjari na kutatua changamoto zote zinazowakabili wadau wa Ukimwi katika kuongeza ufanisi wa kuitumikia Jamii inayowazunguka.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.