Kuelekea msimu wa kilimo mwaka 2025/2026 Manispaa ya Ilemela kupitia Divisheni ya kilimo,Mifugo na Uvuvi leo tarehe 29/09/2025 imeendesha mafunzo kwa maafisa ugani kilimo wai ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha maafisa ugani pamoja na wadau wa kilimo juu ya mabadiliko ya tabia nchi na uwepo wa mvua za vuli za wastani hadi chini ya wastani kwa kipindi cha mwezi Oktoba - Disemba 2025 ili waweze kuwasaidia na kuwashauri wakulima waweze kulima mazao ya muda mfupi na yanayoweza kuhimili ukame pia watumie mbegu zilizo na ubora na zenye uzalishaji mkubwa.
"Lengo letu ni utabiri huu wa hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi yatuelekeze namna gani tutawasaidia wakulima kujua mazao gani walime na kwa wakati gani wapande ili kukabiliana na mabadiliko haya ya tabia nchi na waweze kunufaika na kilimo chao” James Wembe Afisa kilimo.
Naye ndugu Agustino Nduganda Meneja TMA kanda ya Ziwa alitoa mwelekeo wa mvua za vuli za mwaka huu 2025 kuwa zinatarajia kuanza kunyesha wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba na zitakua mvua za wastani hadi chini ya wastani tofauti na ilivyozoeleka. Kwa kawaida wastani wa mvua katika miezi ya Oktoba-Desemba kwa wilaya ya Ilemela ni kati ya milimita 360 hadi 410.
Bi. Grace Minja Afisa kilimo kata ya Kiseke kwa niaba ya washiriki amewashukuru wawezeshaji wa mafunzo kwani yamewawezesha kuweza kwenda kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kuelekea msimu huu wa kilimo na kuwashauri wakulima wafate kanuni bora za kilimo na kuweza kupata uzalishaji wenye tija.
Mafunzo hayo ni hatua muhimu katika juhudi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, huku yakilenga kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii wananchi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.