Zaidi ya shilingi bilioni 18 za kitanzania zinatarajia kutumika katika ujenzi wa barabara za Manispaa ya Ilemela kwa kiwango cha lami.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 08/06/2018 na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga kwenye hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara kati ya Manispaa ya Ilemela na kampuni ya Synohydro Ltd ya China.
Ujenzi wa barabara hizo zenye jumla ya urefu wa kilomita 12.1 utahusisha barabara ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu(Kilomita 9.7), Isamilo-Mjimwema(Bigbite, Kilomita 1.2)makutano ya barabara ya Makongoro-Mwaloni Kirumba(Kilomita 1.2) halikadhalika pamoja na uwekaji wa taa za barabarani na mabirika ya kukusanyia taka.
Akitoa neno la shukrani katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Mstahiki meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga amesema kuwa hadi sasa shilingi za kitanzania milioni 436 kati ya shilingi milioni 636 zimelipwa fidia kwa wananchi kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri .
Mwakilishi wa kampuni ya Sinohydro Ndugu Jia Bin amesema kuwa ujenzi wa barabara unatarajiwa kuanza Juni 15 mwaka huu, ambapo utatekelezwa ndani ya miezi 15 na kuahidi kuwa watahakikisha wanamaliza kwa wakati uliokusudiwa na utajengwa kwa ubora wa hali ya juu.
Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia utiaji saini mkataba wa barabara hizo wamepongeza hatua hiyo na kusema kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizi kutasaidia kurahisisha usafiri kwa wananchi na mizigo hususani kata ambazo mradi unapita pamoja na kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii kama vile shule, hospitali na masoko.
Mradi wa ujenzi wa barabara hizi unagharimiwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia chini ya mradi wa uendelezaji Miji na Majiji “Tanzania Strategic Cities Project”.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemella Renatus Mulunga (Aliyeketi) akitia saini
mkataba wa ujenzi wa barabara za Manispaa ya Ilemela
Mkurugenzi John Wanga (mwenye tai) akitia saini mkataba wa ujenzi huku akishuhudiwa na waalikwa
Mstahiki Meya Renatus Mulunga (Katikati) pamoja na mwakilishi wa kampuni ya synohydro (Upande wa kushoto) Ndg. Jia Bin
pamoja na Mkurugenzi John Wanga(Upande wa kulia)wakipongezana mara baada ya kusaini mkataba
Kutoka kushoto ni mwakilishi wa kampuni ya Sinohydro Corporation Jia Bin,
Mstahiki Meya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga pamoja na
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo John Wanga wakionyesha mkataba wa makubaliano kwa wananchi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.