Wito umetolewa kwa viongozi wa dini Wilayani Ilemela kuwa mstari wa mbele katika kuwahubiria waumini wao habari za upandaji miti na utunzaji wa mazingira kwa ujumla wake.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Ndugu Saidi Kitinga ambae ni katibu Tawala ametoa wito huo wakati wa zoezi la upandaji wa miti lilifanyika katika shule ya Msingi Buswelu
“Utunzaji wa mazingira unahusu jamii nzima,sehemu sahihi ya kupeleka elimu hii ya mazingira ni kwa waumini wa dini zote, waambiwe ukweli kwamba uharibifu wa mazingira ni dhambi kwani unaathiri uhai wa binadamu na viumbe hai vilivyopo.” Amesema Kitinga
Aidha Ndugu Kitinga ameitaka kamati ya amani Ilemela kuwajibika katika masula ya utunzaji wa mazingira na kuandaa kampeni za ushawishi kwa kutambua kuwa mazingira salama ndio uhai wa watu wote.
Nae Mchungaji kiongozi Elisha Msanifu wa kanisa la Highway of Holiness Church (HCC) Buswelu amesema kuwa kanisa hilo lina mpango wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe.Samia Suluhu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira ya taifa hili.
“Sisi kama kanisa tunaandaa kampeni ya utunzaji wa mazingira ambayo itahusisha masuala ya upandaji miti ,tukiwa tayari tutatoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya Wilaya.”Amesema Mchungaji Elisha.
Katika zoezi hilo jumla ya miti 200 imepandwa ambayo ilitolewa na wakala wa misitu Tanzania (TFS) likiongozwa na Ndugu Said Kitinga kwa kushirikiana na balozi wa mazingira Mrisho Amos Mabanzo maarufu kwa jina la “Mr.Tree” kutoka ofisi ya makamu wa Rais wa Tanzania katika kampeni ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.