27 YA KIJANI; MITI 2,361 IMEPANDWA WILAYANI ILEMELA
Katika kuunga juhudi za Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za utunzaji na uhifadhi wa mazingira, wilaya ya Ilemela imefanikiwa kupanda miti 2,361 katika maeneo mbalimbali ikiwa ni ishara ya kumtakia kheri katika siku yake ya kuzaliwa.
Akiongoza zoezi la upandaji miti lililofanyika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilemela mapema tarehe 27 Januari, 2026, Mhe. Said Mtanda, mkuu wa mkoa wa Mwanza ametoa wito kwa wananchi kupanda miti katika makazi yao ikiwa ni sehemu ya uhifadhi wa mazingira.
“Uhifadhi wa mazingira ni kitendo cha kizalendo, kupanda miti ni sehemu ya ibada, iwe miti ya kivuli au miti ya matunda na unapopanda mti leo itakuwa ni faida kwa vizazi vya baadae” alisisitiza Mhe. Mtanda
Naye, mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe. Amiri Mkalipa kwa niaba ya wananchi wa Ilemela alimtakia kheri Rais Samia katika siku yake ya kuzaliwa na kumhakikishia kuwa watumishi wa wilaya hiyo wanamuunga mkono kwa kuchapa kazi na kuhakikisha amani na usalama unakuwepo, ukusanyaji wa mapato, utatauzi wa migogoro na kuwasikiliza wananchi kila mmoja kwa nafasi yake.
Aidha, Mhe. Mkalipa alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuleta fedha nyingi zilizosaidia uboreshaji wa miundombinu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo akitolea mfano wa ujenzi wa soko la kimataifa kirumba pamoja na barabara zake pamoja na ujenzi wa shule za msingi.
Mhe. Mkalipa alihitimisha kwa kusema kuwa zoezi la upandaji miti katika wilaya ya Ilemela lilishaanza mapema kwa kupanda miti ya matunda kwa ajili ya kivuli na kuhamasisha lishe bora.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.