Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu amekabidhi vyeti vya pongezi kwa watoto wa halaiki walioshiriki zoezi la mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024 katika wilaya ya Ilemela ikiwa ni ishara ya kuwashukuru kwa kazi nzuri walioifanya ya kusherehesha na kutoa jumbe mbalimbali za mwenge.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti hivyo iliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo Bi.Ummy amewapongeza watoto hao kwa kujitoa kwao na kutumika kama kichocheo cha ushindi uliopatikana kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuwa washindi wa 9 kitaifa kati ya Halmashauri 195 za Tanzania.
"..muendelee kuwa wasikivu kwa walimu wenu kwa kuzingatia elimu ya uraia mnayoipata muimarishe upendo,umoja na uzalendo.Mkifika nyumbani mkaawaambie wazazi tunashukuru kwa kuwaruhusu kuwa sehemu ya mafanikio yetu.Tunawapenda sana.."
Nae mratibu wa mwenge wa Manispaa hiyo Bi.Lucy Matemba amesema jumla ya watoto wa halaiki 200 kutoka shule za msingi na sekondari ndani ya Manispaa ya Ilemela walishiriki kwa kucheza,kuchora alama mbalimbali za kitaifa kwa ubunifu mkubwa huku akiwasihi watoto hao kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Abubakar Makene ni skauti masta na mkufunzi wa halaiki hiyo yeye anapongeza uongozi wa Ilemela kwa kuona na kutambua mchango wa watoto hao wa halaiki huku akiahidi kuwafanya bora zaidi kwa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka huu wa 2025 .
Wakitoa shukrani zao za dhati kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Emmaculata Mbuta ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Mwinuko na Alan Anderson mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Ziwani wamemshukuru kwa kuwaandalia hafla hiyo ya kuwapongeza huku wakiahidi kuendelea kuwa kichocheo cha ushindi wa namba moja kwa Manispaa hiyo kwa mbio za mwenge wa uhuru zijazo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.