Umoja wa wenza wa viongozi unaojulikana kama ladies of new millenium group ukiongozwa na Bi. Tunu Pinda ambaye ni mwenyekiti wa umoja huo wamepongeza juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini
Wametoa pongezi hizo tarehe 25 Juni, 2025 walipotembelea shule ya sekondari ya Igogwe iliyopo kata ya Bugogwa ndani ya Manispaa ya Ilemela shule ambayo imejengwa kupitia fedha za mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF).
Aidha wenza hao walibainisha lengo la ziara yao kuwa ni kujenga ufahamu. na uelewa kuhusu maendeleo na mafanikio ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa kunusuru kaya za walengwa (TASAF)
Pamoja na ukaguzi wa mradi huo wa shule wenza hao wa viongozi walipata fursa ya kukagua bidhaa za wajasiriamali ambao wapo katika mpango na kusema kuwa wamevutiwa na namna mradi wa TASAF ulivyoweza kuwainua kiuchumi na kuwataka wanufaika hao waendelee na juhudi ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuziongezea thamani.
Kwa niaba ya mkurugenzi wa TASAF Taifa, Bw. Japhet Boaz ameupongeza uongozi wa manispaa ya Ilemela kwa usimamizi mzuri wa miradi ya TASAF hususan ujenzi wa shule ya Igogwe ambao unawanufaisha wanafunzi zaidi ya 700 na kati yao wanafunzi 73 wanahudumiwa na mradi wa TASAF kwa kuwaendeleza kielimu huku akiahidi kuendelea kuwashika mkono katika mradi mwingine ukiwemo ujenzi wa bwalo la chakula.
Kaimu mkuu wa shule Mwl. Uswege Asagwile Mwakalobo akisoma taarifa ya mradi huo amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kwa kiwango cha juu na katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili kwa mwaka uliopita Igogwe imetoa mwanafunzi bora kiwilaya.
Sambamba na ukaguzi wa miradi hiyo ya TASAF, umoja huo wa wake wa viongozi walitumia fursa hiyo kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kutoa msaada wa mitungi 25 ya gesi kwa wanawake na wanaume wanaojishughulisha na shughuli za kupika vyakula ( baba na mama lishe) wanaotoka kwenye vikundi mbali mbali vya wajasiriamali ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan juu ya matumizi ya nishati safi.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa nishati hiyo ya gesi ya kupikia Bi. Mwanaidi Ramadhani mkazi wa kata ya Igogwe wamewashukuru kwa ujio wao na kwa kuwajali wajasiriamali wadogo kwani kupitia nishati hiyo wataepukana na changamoto ya moshi unaotokana na kuni za kupikia pamoja kurahisisha shughuli za jikoni.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.