Wenyeviti wa mamlaka za Serikali za mitaa wamesisitizwa kuhakikisha wanaitisha mikutano ya hadhara kwaajili ya kuhamasisha maendeleo, kutoa taarifa za mapato na matumizi ili wananchi wajue kinachofanywa na Serikali yao.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa mkutano wake wa hadhara katika viwanja vya msitu wa Kipeja kata ya Mecco alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo ambapo akawataka wenyeviti wa mitaa kuhakikisha kila mwananchi anashiriki shughuli za maendeleo pamoja na kutambua kila kinachoendelea ndani ya eneo lake ili kuweka urahisi wa kuchangia miradi na kuimilikisha kwa jamii
'.. Niwasihi wenyeviti wa mitaa japo muda uliobaki ni mchache hakikisheni mnawasilisha taarifa za mitaa, usije kuingia kwenye shida, usije ukakosa kura, someni mapato na matumizi ..' Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula akawataka wananchi wa kata hiyo kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha za miradi ya maendeleo pamoja na kuwakumbusha namna wilaya hiyo inavyofanya vizuri katika sekta ya ardhi kwenye zoezi la urasimishaji na umilikishaji nchini
Godlisten Kisanga ni diwani wa kata ya Mecco mbali na kumshukuru na kumpongeza Mbunge huyo kwa namna anavyohamasisha maendeleo akaongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni 75 kimetolewa kwa kata yake na kujenga madarasa 3 ya shule ya sekondari Nundu, milioni 14 imetolewa kwaajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, matofali 2500 yametolewa na mbunge huyo kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya kata yake pamoja na mifuko 200 itakayotumika kujenga barabara ya mwambani hivyo kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana katika maendeleo
Nae mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa Elimu msingi Mwalimu Marco Busungu akasema kuwa manispaa iko teyari kushirikiana na wananchi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia sera na kauli mbiu ya wilaya hiyo ya Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga ambapo wananchi wanaanzisha mradi, Mbunge atatoa matofali ya ujenzi wa mradi huo na mkurugenzi wa manispaa kumalizia mradi
Kamau Levis na Josephine Chilana ni wananchi wa kata hiyo ambapo wamelalamikia makampuni yanayofanya kazi ya urasimishaji wa makazi ndani ya mtaa wao kushindwa kutimiza wajibu wao kwa wakati hivyo kusababisha kuchelewa kumiliki ardhi yao na kujikwamua kiuchumi jambo lililopata ufumbuzi kutoka kwa Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kuagiza afisa mipango miji kufika eneo la wananchi na kupata suluhu
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula yupo jimboni akiendelea na ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi akishirikiana na wakuu wa idara za manispaa ya Ilemela na wakuu wa taasisi zilizopo ndani ya wilaya hiyo ikiwemo Tanesco, MWAUWASA na TARURA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.