Baraza la wazee la Wilaya ya Ilemela likiongozwa na mwenyekiti wake Mzee Yusuph Mohamed limefanya kikao cha kawaida kujadili masuala yanayowahusu ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama ,upatikanaji wa huduma zinazotolewa na serikali kama vile mikopo na huduma za afya .
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika kata ya Bugogwa mratibu wa wazee Wilaya ya Ilemela Bi.Neema Kavishe amesema wazee ni tunu ya kujivunia mahali wanapokuwepo kwani busara nyingi zinazopatikana na kutolewa katika jamii zimetokana na wao huku akiiasa jamii ya Ilemela kuendelea kujivunia na kuwaheshimu wazee kwa kuwajali na kuwapatia mambo yote yenye tija kwao yanayowezekana kufanyika katika nyakati zao za uzee .
Fidelis Kilaryo ni mratibu wa iCHF wilaya ya Ilemela yeye ametoa elimu kuhusu bima ya afya iliyoboreshwa (iCHF) ambapo amesema bima hiyo ilianzishwa na serikali ya Tanzania chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na wizara ya Afya na wizara ya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto huku akiwatoa hofu juu ya uhalali wa uwepo wa bima hiyo na kuwasihi waitumie kwa kuzingatia zake.
“.. faida za bima hii ni pamoja kuleta kiwango fulani cha usalama wa kifedha na utulivu ,ni malipo kidogo kwa watu wengi . Mhusika atatakiwa kulipa shilingi elfu 30,000 kwa kaya ya watu 6 kwa mwaka ..”
Mzee Saulo Msumari mkazi wa Bugogwa ni mmoja wa wajumbe ndani ya baraza la wazee Ilemela ameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuwa na utaratibu wa kuwakumbuka kwa kuendesha vikao vya mara kwa mara na kuahidi kuwa balozi mzuri kwa wazee wengine.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.