Mhe Said Mtanda mkuu wa mkoa wa Mwanza, ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanashirikiana na walimu katika malezi ya wanafunzi kwani wanafunzi hutumia muda mwingi wakiwa shuleni kuliko nyumbani.
Rai hiyo aliitoa wakati wa hafla ya makabidhiano ya ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa iliyofanyika katika shule ya sekondari Lumala iliyopo kata ya Ilemela siku ya Ijumaa tarehe 12 Julai 2024
Aliongeza kusema kuwa wazazi wanapaswa kuelewa kuwa asilimia 80 ya muda wa wanafunzi wanaishi na walimu, kwa hiyo malezi yao yanatoka kwa walimu hivyo ni muhimu walimu wakapewa ushirikiano ili kuweza kuwa na kizazi chenye nidhamu na maadili sambamba na kuwataka wazazi kuwa karibu na wao na kufuatilia mienendo yao ya kila siku.
“Kumeibuka wimbi kubwa la wazazi kuandamana jambo ambalo sio sawa, pale mwalimu anapotoa adhabu kwa mujibu wa sheria kwa nia ya kumuonya mwanafunzi, mnapaswa kushirikiana na walimu katika malezi”alisema Mhe Mtanda.
Aidha aliwakumbusha walimu kuhakikisha kuwa adhabu watakazotoa kwa wanafunzi zizingatie sheria za nchi na si vinginevyo.Huku akiwataka walimu kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana na serikali kwani serikali inaendelea kufanya mambo mazuri kwasababu hakuna elimu bora bila walimu bora, alisema.
Pamoja na hayo aliwataka wanafunzi kuhakikisha wanaitumia fursa ya uwepo wa mazingira bora ya kujifunzia kwa kusoma kwa juhudi ,maarifa na bidii ili kuweza kufikia azma na malengo yao.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Lumala kwa niaba ya wanafunzi wa manispaa ya Ilemela wameahidi kuwatii walimu na wazazi ikiwa ni Pamoja na kusoma kwa bidii kutimiza ndoto zao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.