Wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia mlo kamili wenye virutubisho vyote vinavyohitajika katika makuzi na afya ya binadamu hasa kwa vijana wanaokua
Rai hiyo imetolewa na mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa elimu msingi takwimu Mwalimu Johanes John wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya lishe duniani kiwilaya yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buswelu yakipambwa na kauli mbiu ya ‘ Lishe bora kwa vijana balehe, Chachu ya mafanikio yao’ ambapo amewataka wazazi na walimu kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa lishe na afya katika aina ya vyakula kwaajili ya kuukinga mwili dhidi ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza ili vijana waweze kukua vizuri na kulitumikia vyema taifa lao
‘.. Tafiti mbalimbali zimefanyika na kutokana na tafiti hizo imeonekana watu tunapata chakula lakini hatupati chakula bora kwaajili ya manufaa ya miili yetu na akili yetu na kama hatuli vizuri lazima tuelimishane namna bora ya aina ya chakula, Baada ya siku ya leo tusikilize ushauri wa wataalam wetu na rika hili la vijana balehe ndio rika kusudiwa sababu rika hili linataka akili nzuri iliyotulia hivyo lazima ale vizuri ..’ Alisema
Aidha Mwalimu Johanes ameongeza kuwa ni wajibu wa wazazi na walezi kwenda kusimamia utaratibu wa lishe kwa vijana wao pindi wanapokuwa majumbani na kuasa kutopuuzwa kwa elimu ya lishe inayotolewa na wataalam
Kwa upande wake mratibu wa lishe manispaa ya Ilemela Bi Pili Kasimu amefafanua kuwa kwa robo ya kwanza ya Julai-Septemba 2023/2024 vijana waliopatiwa elimu ya ulaji unaofaa na kufanyiwa tathimini ya hali ya lishe ni 390 ambapo vijana 111 sawa na asilimia 28.5 walikuwa na hali nzuri ya lishe, vijana 179 sawa na silimia 45.9 walikuwa na uzito uliozidi, vijana 61 sawa na asilimia 15.6 walikuwa na uzito uliokithiri pia vijana 39 sawa na asilimia 10 walikuwa na uzito pungufu pamoja na kukabiliwa na changamoto za vijana kutozingatia muda wa kula chakula na kujikita katika anasa mbalimbali ikiwemo kuangalia luninga, ushiriki mdogo wa kina baba katika malezi na makuzi ya vijana balehe, vijana kupendelea vyakula visivyofaa na kuchangia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo chips na soda
Getruda Cosmas ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kaselya ambapo yeye ameshukuru kwa maadhimisho hayo kufanyika katika shule yao pamoja na kupongeza zoezi la upimaji hali za lishe lililofanywa na wataalam wa manispaa ya Ilemela katika kilele cha maadhimisho hayo pamoja na kuomba zoezi hilo liwe endelevu badala ya kusubiria shughuli za maadhimisho za kila mwaka
Wilaya ya Ilemela inajivunia mafanikio ya kupungua kwa kiwango cha utapiamlo ambapo kwa mwaka 2021/2022 utapiamlo ulikuwa asilimia 3 na sasa mwaka 2022/2023 utapiamlo ni sawa na asilimia 2.9
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.