Kupitia maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIM) yanayofanyika kila robo ya mwaka, wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia lishe bora kwa watoto kwani ndio msingi wa makuzi bora na kuwasaidia kuepukana na magonjwa mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa lishe bora kama vile udumavu na utapiamlo.
Rai hiyo imetolewa na Bi Pili Kassim ambae ni afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela wakati wa utoaji wa elimu ya lishe katika mtaa wa Ng’wang’wila uliopo kata ya Sangabuye.
Elimu hiyo ilienda sambamba na ugawaji wa miche ya viazi lishe kwa ajili ya kupanda na kuweza kuwasaidia upatikanaji endelevu wa zao hilo muhimu kwa afya na makuzi ya watoto na jamii kwa ujumla.
Aidha pamoja na maadhimisho hayo ya SALIM, jumla ya watoto 396 waliogundulika na tatizo la ukosefu wa lishe kutoka kata nne za Manispaa ya Ilemela ambazo ni Sangabuye, Kayenze, Shibula na Bugogwa wanatarajia kunufaika na msaada wa unga wa viazi lishe kutoka shirika lisilo la kiserikali SOS children’s village lililojikita kusaidia vizazi vya watoto kuwa na maisha bora
Maadhimisho hayo ya siku ya lishe ya mtaa (SALIM) yanaendelea katika mitaa yote 171 ya Manispaa ya Ilemela hivyo wazazi na walezi wanahimizwa kujitokeza kupata elimu bora ya lishe.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.