Na PASCHALIA GEORGE, AFISA HABARI ILEMELA
Mashindano ya kombe maalum la watoto wenye ulemavu wa akili ‘’Special Olympics’’ambayo yalihusisha mchezo wa riadha,mpira wa mikono na mpira wa miguu yamefungwa leo kimkoa ambapo wilaya zote nane za mkoa wa Mwanza zimeshiriki huku Halmashauri ya manispaa ya Ilemela ikiibuka kidedea katika mchezo wa mpira wa miguu bila kupoteza mechi ya michezo yote.
Akizungumza wakati wa kufunga michezo hiyo mgeni rasmi katika mashindano hayo ambaye pia ni Afisa michezo mkoa wa Mwanza James William Ngasa amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalum wasiwafiche ndani kwa kuona aibu au kuhisi imani potovu juu ya ulemavu wowote ambao mtoto anao.
“Watoto wote wana haki sawa,jamii inapaswa kuelewa hata wenye ulemavu wana haki pia.Wazazi msiwafiche watoto wenye ulemavu watoeni washiriki na wenzao michezo ni tiba ya akili wanapojumuika na kubadili mazingira mara kwa mara akili zao huchangamka na wakati mwingine wasio na ulemavu mkali wa akili hupona kabisa na kumuwezesha mtoto kukua vizuri na kuendelea na majukumu kama watoto wengine wasio na ulemavu.”amesema Ngasa
Nae afisa elimu maalum wa manispaa ya Ilemela Sarah Ulimboka amesema tunafahamu changamoto nyingi walizonazo watoto wenye ulemavu hivyo sisi jamii tunao wajibu wa kuwapenda na kuwajali watoto hawa kwa kuwapatia mahitaji yao ya msingi kwa wakati.
“Natoa shukrani za dhati kwa uongozi wa manispaa ya Ilemela kwa kuendelea kujali uwepo wa watoto hawa kwa kutoa misaada mbalimbali na kualika wadau kuwasaidia mahitaji katika makuzi yao,tunashukuru walimu wanaowalea watoto wenye ulemavu mbalimbali pamoja na changamoto zilizopo bado tunaweza kusimama imara kuwafundisha na kuwalinda.”amesema Ulimboka.
Mashindano haya maalum yamemalizika kwa ngazi za wilaya na sasa timu ya mkoa wa Mwanza inayoundwa na jumla ya wachezaji 50 kwa michezo mitatu mpira wa mikono,riadha na mpira wa miguu ishapatikana itakayocheza ngazi ya taifa.Kati ya wachezaji hao 50 wachezaji 10 wametoka timu za manispaa ya Ilemela.Michezo hiyo kitaifa inatarajiwa kuanza kuchezwa hivi karibuni mkoani Mwanza .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.