Afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasim amewaasa kina mama ambao ndio walezi wakuu wa watoto na jamii kwa ujumla kufuatiilia mienendo ya afya za watoto wao kwa kuzingatia kuwa uimara wa afya nzuri katika ukuaji wa watoto ndio unaozalisha vijana na viongozi imara ndani ya jamii na taifa kwa ujumla.
“..Tuungane katika kampeni hii ya kitaifa ya mwezi wa afya na lishe ya mtoto katika kumpatia mtoto huduma zote muhimu za afya.Wazazi na walezi kila mmoja anawajibika kufuatilia afya ya mwanae ..”
Akizungumza na kina mama waliotokeza kupata huduma mbalimbali za kliniki katika zahanati ya Nyerere iliyopo kata ya Buswelu ndani ya Manispaa ya Ilemela Bi.Pili ametaja huduma zinazotolewa ni pamoja na utoaji wa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto wenye umri kuanzia mwaka mmoja hadi miaka minne na miezi 11 ,matone ya Vitamin A pekee kwa watoto kuanzia miezi 6 hadi miezi 11 sambamba na tathmini ya hali ya lishe kwa watoto wenye umri kuanzia miezi 6 hadi 59.
Ameongeza kuwa huduma zote zinatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kampeni hiyo inafanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 01-31 ,Desemba 2024 huku akibainisha kuwa Halmashauri imekusudia kuwafikia jumla ya watoto 66,486 ambapo hadi kufikia jana tarehe 19,Desemba 2024 watoto waliofikiwa ni 58,980 sawa na asilimia 88.7 ya lengo.
“..tunazidi kuwahamasisha kina mama na kina baba kuwaleta watoto wao kupata huduma hizi za afya,na kwale ambao hawajakamilisha chanjo zingine waje ,tupo hapa kuwahudumia..” Amesema Jenifer Stephano Muuguzi katika zahanati ya Nyerere
Jamila Khalid ni mmoja wa kina mama waliohudhuria kliniki hapo yeye anashukuru Halmashauri kwa kuendelea kutoa elimu juu ya afya ya mtoto na lishe huku akisisitiza elimu hiyo iende mbali zaidi hasa maeneo ya nje ya mji.
“...Kuna watu maeneo mengine tangu mama anashika ujauzito mpaka anajifungua hajawahi kufika kliniki,kwa mtu wa namna hiyo haya mambo ya matone sijui kama ataelewa.Mfike na huko nje nje jamii nzima tuwe na uelewa wa pamoja..”
Kampeni ya kitaifa ya mwezi wa afya ya mtoto na lishe kwa mwaka huu 2024 imepambwa na kauli mbiu isemayo matone ya vitamini A ni bora kwa mtoto wetu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.