Timu ya wawezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF Manispaa ya Ilemela imeaswa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu mkubwa na unyenyekevu na kuweka uzalendo mbele ili walengwa wa mpango huo waweze kupata huduma bora na sahihi.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii manispaa ya Ilemela Ndugu Sitta Singibala akimuwakilisha mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary wakati wa kikao kazi cha kusikiliza changamoto na kujengeana uwezo wawezeshaji hao.
“Shughuli hii inataka muhusika awe muadilifu kiasi cha kutosha kwa sababu tunaenda kufanya zoezi linalohusiana na fedha na upo mwenyewe, tukumbuke pesa inataka uadilifu mkubwa”, Amesema
Aidha Ndugu Singibala akasisitiza wawezeshaji kuwa wasikivu na wanyenyekevu kwa walengwa wataofuata huduma ikiwemo kutatua changamoto watakazoziwasilisha pamoja na kutumia lugha rahisi itakayoeleweka kwa haraka ili mpango huo uweze kuwa na tija iliyokusudiwa
Kwa upande wake mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF Manispaa ya Ilemela Bwana Leonard Robert amewataka wawezeshaji hao kuhakikisha wanaweka jitihada katika kupunguza idadi ya walengwa wanaopokea fedha taslimu mkononi badala yake waweze kutumia benki, simu au wakala kutoka idadi ya watu 1577 kwa sasa kufikia angalau watu 500 sambamba na kuhakiki majina halisi ya walengwa na yale yaliyo katika namba za simu wanazotumia kupokelea fedha
Davis Ulotu ni miongoni mwa wawezeshaji waliohudhuria kikao hicho ambapo ameshauri wawezeshaji wanaohudumia mtaa wa Bezi kata ya Kayenze eneo la kisiwa kutangulia eneo hilo siku moja kabla tofauti na wawezeshaji wa maeneo mengine ili kuongeza ufanisi wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto ya usafiri
Kiasi cha shilingi Milioni 277.59 kinatarajiwa kutolewa kwa kaya 5682 ikiwa ni malipo kwa ajili ya kipindi cha Mwezi Novemba na Disemba awamu ya 12.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.