Watu wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa UKIMWI wameshauriwa kujikubali na kuendelea na shughuli za kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu mwenyekiti wa kamati ya UKIMWI ya manispaa ya Ilemela Mhe Sara Ng’wani wakati wa ziara ya kamati hiyo kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa shughuli zinazosimamiwa na kamati ndani ya manispaa hiyo ambapo amezipongeza taasisi zinazotoa huduma kwa WAVIU pamoja na kulitaka kundi hilo kutojinyanyapaa na kuendelea na utekelezaji wa shughuli za uzalishaji mali ili liweze kujitegemea na kujisimamia.
‘.. Niwatie moyo, kuishi na virusi vya UKIMWI sio ulemavu mnaweza mkafanya shughuli nyingine zozote za kiuchumi kama watu wengine na mkajikomboa kiuchumi ..’ Alisema
Aidha Mhe Ng’wani amezitaka taasisi zinazotekeleza shughuli za kudhibiti UKIMWI ndani ya wilaya ya Ilemela kuhakikisha zinashirikiana na viongozi wa maeneo husika ili kurahisisha utatuzi wa changamoto za wananchi.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Bi Angeline Juma amelipongeza shirika la UNTOLD kwa kutoa elimu ya afya ya mwili na kiroho kwa wateja wake sanjari na kuasa taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Anitha Dotto ni msimamizi wa miradi kutoka taasisi ya Wadada Solutions ambapo amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi yake ikiwemo uelewa mdogo wa jamii juu ya masuala ya ukatili na namna unavyochangia kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI huku Bi Stella Patrick akiishukuru kamati kwa kuwatembela kuona namna wanavyonufaika na misaada inayotolewa na taasisi zinazopambana na UKIMWI na ukatili.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.