WAUGUZI ILEMELA WAADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI KWA KUTOA HUDUMA ZA AFYA.
Wauguzi wa halmashauri ya manispaa Ilemela wamefanya sherehe za kuadhimisha kilele cha siku ya wauguzi duniani ambayo hufanyika mwezi Mei, 12 ya kila mwaka iliyotanguliwa kwa kutoa huduma za afya sehemu zote zenye changamoto kubwa kama Visiwa vya Bezi na Kituo cha afya Buzuruga
Akizungumza katika hadhara hiyo mgeni rasmi na mkurugenzi wa manispaa Ilemela John Wanga mbali na kuwapongeza kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua changamoto zinazowakabili na kuwataka kuwa wavumilivu wakati hatua hizo zikiendelea kuchukuliwa kwa kuhakikisha yanakuwepo mazingira rafiki katika kutoa huduma za afya
“Ndugu zangu zipo changamoto za kisera na hizi za kawaida ambazo zipo ndani ya uwezo wa ofisi yangu niwahakikishieni kuwa tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunazitatua ila niwaombe muwe wavumilivu kwani si rahisi zote kuisha kwa siku moja” Alisema
Aidha amewataka wauguzi kuendelea kujituma katika kutoa huduma sambamba na kuwa waadilifu katika kazi yao na kuhitimisha kwa kutoa shilingi za kitanzania laki moja kwa kila muuguzi mstaafu aliyeshiriki sherehe hizo.
Nae Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Daktari Leonard Masale alisema kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha wanaboresha huduma za afya huku akiwaasa juu ya umuhimu wa umoja na mshikamano.
Kwa upande wao wauguzi wakiwakilishwa na mwenyekiti wa chama cha wauguzi Ilemela Bi Assumpta Mwijage mbali na kumshukuru mgeni rasmi na viongozi alioambatana nao wameahidi kuwa wataendelea kuzingatia uadilifu na ueledi wa kazi yao katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Mwanza hoteli na zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa wilaya Ilemela Mhe Dkt Leonard Masale, Mkurugenzi wa Ilemela John Wanga, katibu wa mbunge jimbo la Ilemela Kheri James, Wauguzi wastaafu na wauguzi wote wa wilaya Ilemela wakiongozwa na muuguzi mkuu Bi Kalunde Gisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.