Watumishi wa Umma ngazi ya watendaji wa mitaa na kata ndani ya manispaa ya Ilemela wamejengewa uwezo kwa kupata mafunzo yatakayowasaidia kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kutoa huduma bora kwa wananchi wao
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Morning Star kata ya Ilemela Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bi Neema Semaiko amefafanua kuwa mafunzo yanayotolewa yakawe chachu katika uboreshaji wa utoaji huduma kwa wananchi pamoja na utendaji mzuri wa kazi za Serikali unaozingatia sheria, kanuni na sera mbalimbali
'.. Kuna watu wameajiriwa wanalipwa mishahara kwa kazi ya kukufuatilia wewe utendaji wako wa kazi, Kwahiyo lazima tuwe waadirifu katika utendaji wetu wa kazi, Lazima tufanye kazi kwa sheria, kanuni na taratibu, Tusifanye shida za wananachi kuwa fursa ya kujipatia fedha zisizohalali ..' Alisema
Aidha Bi Semaiko amewataka watumishi hao kujikinga dhidi ya tatizo la afya ya akili wawapo kazini ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku pamoja na kulinda afya zao kwa maslahi yao binafsi na taifa kwa ujumla
Kwa upande wake afisa utumishi mkuu wa manispaa ya Ilemela Bwana Teulas Egidy akasema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ufahamu wa nini wanatakiwa kukifanya wawapo katika utumishi wa umma, changamoto gani wanaenda kukutana nazo na kwa namna gani wataenda kuzitatua sanjari na kutambua mipaka ya nafasi zao pamoja na kipi chakufanya na kipi si chakufanya kulingana na vyeo vyao
Dkt Garvin Kweka kutoka chuo kikuu cha Muhimbili ambae pia mtaalam mbobezi wa Figo, magonjwa ya ndani na afya ya akili ni miongoni mwa wakufunzi katika mafunzo hayo ambapo amesisitiza kuwa watendaji hao wanakwenda kuongoza watu ambao hawafikirii kwa kufanana na kwamba jamii kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya afya ya akili hivyo kuwasisitiza kuwa makini na kufanya kazi kwa kufuata sheria badala ya utashi binafsi usiozingatia kanuni na taratibu za Serikali
Ndugu Nhkilo Elias ni mtendaji wa kata ya Kitangiri na Bi Nicetha Binomugamizi Victor ni mtendaji wa mtaa wa Kigoto kata ya Kirumba ambao kwa nyakati tofauti wamempongeza na kumshukuru mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu kwa kuamua kutoa mafunzo hayo kwao kwa kuwa yatawaongezea ujuzi ambao hawakuupata darasani kulingana na taaluma zao na kuongeza ufanisi katika utoaji wao wa huduma za kila siku kwa wananchi wa maeneo yao pamoja na kuwaasa wenzao kuzingatia na kuyafanyia kazi mafunzo wanayoyapata
Manispaa ya Ilemela inaendesha mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wote wa mitaa na kata zake kupitia mradi wa Green and Smart City .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.