Watumishi wa idara ya afya wa Manispaa ya Ilemela wameaswa kuwajibika ipasavyo kila mmoja kwa nafasi yake kwa kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kuleta matokeo chanya katika huduma mbalimbali za afya zinazotolewa kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa mganga mkuu wa mkoa Bi.Ester Maliki ambaye pia ni katibu wa afya mkoa wa Mwanza wakati alipohudhuria kikao kazi cha idara hiyo katika ukumbi wa manispaa ya Ilemela kilichohokuwa na malengo ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa huduma za afya zilizotolewa kuanzia Januari hadi Septemba 2023 sambamba na kujadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi na kuboresha huduma hizo.
“Kila mtu awajibike kwa nafasi yake,mvae umiliki wa kila kinachofanyika kwenye maeneo yenu,usimamizi wa miradi mbalimbali ,ukusanyaji na usimamizi wa mapato kwenye vituo vyetu ni jukumu la wote kikubwa ni kugawana majukumu ili mambo yaende kwa mpangilio mzuri.” Amesema Bi.Ester
Pamoja na hilo Bi.Ester ametoa pongezi kwa kazi nzuri inayoendelea katika idara ya afya Manispaa ya Ilemela akaongeza kusema kuwa kazi hii ya huduma za afya ni wito hivyo wazidi kuipenda na kuifanya kwa bidii zaidi ili huduma ziwe bora zaidi.
Nae Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Dkt.Samson Marwa amesisitiza suala la wahudumu wa afya kutoa elimu za masuala ya kiafya kwa jamii hasa hasa masuala ya lishe bora ambayo ndio inamjenga mtu kuwa imara kiakili .
“Jamii inapaswa kufahamu mchanganyo wa makundi matano ya vyakula,wanga,protini,mbogamboga,matunda na sukari na mafuta bila kusahau maji kwa kuzingatia vipimo sahihi vyenye tija sio kula tu mladi kushiba.” Amesema Dkt.Marwa
Sambamba na hayo Dkt.Marwa ametoa wito kwa wahudumu wa afya katika vituo vyote vya kutolea huduma ndani ya manispaa ya Ilemela kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya kuhara na kipindupindu ambayo yameanza kutokea kwa mikoa jirani.
“Kuchukua tahadhari ya kipindupindu ni muhimu na sisi kama wataalam wa afya tunawajibika kuelimisha jamii juu ya majanga hayo hasa nyakati hizi za mvua.”
Bi.Emila Msangi ni katibu wa afya Manispaa ya Ilemela yeye amesisitiza suala la ukusanyaji wa mapato kwa watumishi vituoni na kufanya kazi kwa umoja kwa manufaa ya wote.
“Kadri mnavyokusanya ndivyo mtakavyokuwa huru kutumia kwa matumizi yenu yenye tija katika maboresho ya utoaji huduma vituoni,ipo haja ya kubuni mbinu zaidi za kuwavutia wateja wetu.” Amesema Bi.Emila
Taarifa mbalimbali za kiafya kama vile hali ya lishe,Malaria,kifua kikuu,huduma za ustawi wa jamii zimewasilishwa na kujadiliwa lengo ikiwa ni kuboresha utoaji wa huduma.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.