Manispaa ya Ilemela kupitia idara ya Afya imelenga kutoa chanjo ya matone ya polio kwa watoto 131,828 wenye umri chini ya miaka 5.
Mhe Hassan Masala Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ambae ni Mwenyekiti wa kamati ya afya ya Msingi Wilaya ya Ilemela, amewataka wataalam wa afya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa chanjo ya matone ya polio ili kuweza kuondokana na dhana potofu juu ya chanjo hii.
Ametoa wito huo wakati akiongoza kikao cha kamati ya Afya ya msingi kilicholenga kuongeza uelewa kwa wanajamii juu ya chanjo kwa ajili ya kumlinda mtoto dhidi ya polio kwani ni gonjwa usio na tiba hivyo chanjo ni kwa ajili ya kuimarisha kinga.
Pamoja na wito huo Mhe Masala amewapongeza wataalam wa afya kwa namna wanavyojitoa katika kuhudumia wananchi pamoja na kuwataka kuhakikisha wanakamilisha lengo lililowekwa na Serikali la kuwafikia watoto wote wanaotakiwa kupata chanjo
‘.. Niwatie Ari mtakapoendelea na zoezi hili tutawapa ushirikiano na tupo tayari kushirikiana nanyi kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza kwani tunachotaka ni wananchi wetu wawe salama na sisi tupo kwa ajili ya kulinda usalama wao ..’ Alisema
Mratibu wa chanjo Ndugu Shamte Almasi, ametoa wito kwa wazazi na walezi wasikatae chanjo kwani madhara ya ugonjwa wa polio ni makubwa ambayo yanaweza kupelekea kifo lakini pia watoto kupata ulemavu wa kudumu wa mikono na miguu.
Pamoja na hayo amewataka kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwapatia chanjo watoto hao ili lengo la kutokomeza ugonjwa huu wa polio liweze kufikiwa sambamba na hilo ameomba wazazi au walezi kuacha maelekezo juu ya kampeni hii ili kurahisisha zoezi hili.
Kampeni ya chanjo ya polio itafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 4 mwezi wa kumi na mbili 2022 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi vinavyopatikana katika Manispaa ya Ilemela, nyumba kwa nyumba na maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile sokoni. Sambamba na uchanjaji huduma zingine zitatolewa ikiwemo elimu ya chanjo na kuimarisha huduma za chanjo katika vituo vya kutolea chanjo.
Ikumbukwe Polio ni ugonjwa usiokuwa na tiba na unaosababishwa na virusi vya polio, ugonjwa huu unasababisha kupooza na hatimaye kifo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.