Watendaji wa mitaa ya wilaya ya Ilemela wametakiwa kusimamia bei elekezi ya uuzwaji wa sukari iliyotolewa na serikali ili kuzuia upandishaji holela wa bei ya bidhaa hiyo kutoka kwa wafanya biashara wasio waaminifu na wanaoificha ili isipatikane kwa urahisi kwa wananchi
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi katika viwanja vya ofisi ya kata ya Buswelu ambapo amewataka watendaji kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafanya biashara wote watakaobainika kupandisha bei ya sukari kinyume na maelekezo ya bei elekezi ya serikali.
‘.. Serikali imetoa bei dira na bei dira imetofautiana mkoa kwa mkoa, Kwa mkoa wa Mwanza sukari kilo inapaswa iuzwe shilingi elfu mbili mia sita hamsini mpaka elfu tatu kwa bei ya rejareja, Kwa bei jumla inapaswa kuuzwa shilingi elfu mbili mia nane mpaka elfu tatu na mia mbili, Wako watu wanatumia nafasi hiyo kuendelea kujinufaisha kwa kuuza bei ya juu ambayo ni kinyume ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala mbali na kubainisha shughuli za maendeleo zilizofanywa na serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan amewatoa hofu wananchi wa Ilemela juu ya upatikanaji wa bidhaa hiyo na kwamba serikali kupitia wizara ya kilimo imekwisha toa kibali kwa wafanyabiashara wakubwa kuagiza sukari kutoka nje ya nchi ili kukabiliana na upungufu pamoja na kuwataka maafisa biashara kufuta leseni za biashara kwa wale watakaobainika kupandisha bei kiholela
Paul John na Gilbert Michael ni wananchi wa kata ya Buswelu ambao kwa nyakati tofauti licha ya malalamiko ya bei ya sukari pia wameomba kuharakishwa kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Buswelu senta kupitia Isenga mpaka CocaCola na manispaa kuweka mikakati ya muda mrefu na mfupi katika kuboresha sekta ya elimu
Akihitimisha diwani wa kata ya Buswelu Mhe Sara Ngh’wani amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo kwa utatuzi wa kero za wananchi wake pamoja na kuipongeza serikali kwa fedha za miradi ya maendeleo zilizoletwa ndani ya kata yake huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana katika maendeleo
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.