Ikiwa ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa kidigitali wa anwani za makazi (NaPA), serikali ya Tanzania kupitia ushirikiano wa wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari,Wizara ya Ardhi na maendeleo ya makazi na Ofisi ya Rais TAMISEMI wameungana kuendeleza utekelezaji wa operesheni anwani za makazi iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan mnamo Februari 2022 kwa kutoa mafunzo ya maboresho ya mfumo huo ngazi za Halmashauri.
Akifungua mafunzo hayo yaliyohusisha Wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata na mitaa kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi.Neema Semwaiko amewataka wahudhuriaji wa mafunzo hayo kuwa wasikivu na kulinda taarifa wanazopewa na wananchi.
".. taarifa zinazokusanywa mitaani ni muhimu kwa maendeleo ya Ilemela yetu kidigitali,niwatoe hofu wananchi kuwa taarifa zenu zinatumika kwa matumizi ya kiserikali na zinalindwa.."
Akitoa mafunzo ya mfumo wa NaPA mtaalam wa mfumo huo kutoka wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari Bi.Rehema Chillo ametaja faida za mfumo huo kuwa ni kurahisisha huduma mbalimbali za kijamii kama vile huduma za afya magari ya wagonjwa na magari ya zimamoto yatafika kwa urahisi , huduma za posta na usafirishaji wa vifurushi hadi mahali husika,kuimarisha shughuli za kibiashara sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama kwani eneo na watu wake watakuwa wametambuliwa.
Hosea Emmanuel ni mtendaji wa kata ya Kawekamo yeye anasema ameupokea vizuri mfumo huo kwani utarahisisha utendaji kazi kidigitali ambapo barua za utambulisho wa wananchi katika masuala mbalimbali zinaweza kupatikana ndani ya mfumo huo huku akiwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano katika zoezi la ukusanyaji taarifa mitaani pale zitakapohitajika na kujisajili kupitia mfumo wa NaPA.
Ni malengo ya serikali ya awamu ya sita kuimarisha miundo mbinu ya mawasiliano kwa wananchi wake ili kukuza uchumi wao na kuleta maendeleo ndani ya jamii.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.