Wataalam wa idara ya afya Manispaa ya Ilemela wameshauriwa kuwafikia wananchi kwa ajili ya kuwapa elimu ya umuhimu wa bima ya afya ili waweze kuepukana na gharama kubwa wakati wa matibabu.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Dkt .Angeline Mabula wakati wa mkutano wake wa hadhara katika viwanja vya Kangae 'B' kata ya Nyakato ambapo amesema kuwa ipo haja kwa wananchi kuelewa kwa kina juu ya bima ili iwe rahisi kukata bima hizo .
"..Ni ngumu sana hawa wananchi kukata bima kama hawana uelewa wa kutosha kuwa bima ina faida gani kwao, bahati nzuri hata sisi wawakilishi wao tumeshapitisha sheria ya bima lakini hili halipaswi kuishia katani tu au wilayani, mtenge muda muwafikie wananchi .."Alisema
Aidha Dkt.Mabula amewataka wananchi wa kata hiyo kuwa wavumilivu kutokana na kero ya changamoto za barabara kwa kuwa Manispaa ya Ilemela imeweka mkakati wa ununuzi wa ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa barabara ili kurekebisha barabara za mitaa
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Jeremiah Lugembe mbali na kumpongeza mbunge huyo kwa kazi nzuri anazozifanya amemuhakikishia mbunge huyo kuwa kazi ya uelimishaji juu ya masuala mbalimbali ya afya inaendelea na kwamba mitaa yote itafikiwa.
Lugembe amekiri kutambua makundi mbalimbali yanayopatikana ndani ya manispaa hiyo ikiwemo bodaboda ,wazee na kuahidi ushirikiano na kuwataka kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi .
Lilian Chiguma ni mwakilishi wa mganga mkuu wa Wilaya ya Ilemela ambapo amesema kuwa serikali inaendelea na juhudi katika kuboresha sekta ya afya hivyo kuwaasa wananchi kuiunga mkono na kukata bima za afya ili kuepuka gharama wakati wa matibabu .
Silvanus Manija na Nusra Yahya Ramadhan ni wananchi wa mtaa wa Kangae 'B' ambapo licha ya kumpongeza mbunge wao na Serikali kwa kazi kubwa iliyofanyika wamelalamikia ubovu wa barabara za mtaa huo na kero ya ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo yao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.