Wataalam kutoka idara mbalimbali za manispaa ya Ilemela wametakiwa kushirikiana na kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuimarisha suala la lishe katika jamii
Rai hiyo imetolewa na mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Joanitha Baltazar wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha 2023/2024 katika ukumbi mdogo wa ofisi za mkurugenzi wa manispaa hiyo ambapo amewataka wataalam wote kushiriki katika mapambano ya kuboresha masuala ya lishe katika jamii badala ya kumuachia afisa lishe peke yake
‘.. Suala la lishe si la afisa lishe peke yake, watu wa idara nyengine pia wanaowajibu wa kufanya ili kuimarisha hali za lishe za watu wetu, Lishe ndio maisha lishe ndio kila kitu tukimuachia mtu wa lishe pekee hatuwezi kufika ..’ Alisema
Aidha Bi Joanitha ameagiza kufanyika kwa ukaguzi kwa wazalishaji wa bidhaa za vyakula kama wanazingatia masuala ya virutubisho na lishe ikiwa ni pamoja na kiutoa elimu ili wananchi waweze kupata chakula salama na bora
Kwa upande wake mratibu wa lishe manispaa ya Ilemela Bi Pili Kasim amefafanua kuwa manispaa yake imefanikiwa katika kupunguza changamoto ya utapiamlo kwa wananchi wake pamoja na kuzidi malengo katika utoaji wa chanjo na vitamin kwa watoto
Bi. Hellen Mcharo ni mchumi wa manispaa ya Ilemela ambapo amepongeza utekelezaji wa shughuli za lishe katika manispaa hiyo huku akishauri kuwekwa msisitizo katika kusimamia afua zote za lishe katika mwaka ujao wa fedha
Nae afisa kilimo wa manispaa ya Ilemela Ndugu Dotto Samuel akafafanua kuwa idara ya kilimo imetenga zaidi ya milioni mbili na nusu kwaajili ya kuhamasisha kilimo cha mjini ili kuondokana na upungufu wa vitamin ‘A’ sanjari na kuweka mpango wa kuanzisha mashamba darasa kwa kata za nje ya mji ikiwemo Sangabuye, Kahama, Shibula, Bugogwa, Kayenze na Nyamhongolo ili kuondokana na udumavu
Manispaa ya Ilemela inaendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za lishe ili kuhakikisha sekta ya lishe inazidi kuimarika na wananchi wanakuwa na afya bora kwa maendeleo ya taifa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.