Kuelekea uchaguzi mkuu 2025, mapema leo tarehe 26 Oktoba 2025 jumla wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo 2870 wameapa kiapo cha utii sambamba na kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kusimamia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 oktoba 2025.

Akifungua mafunzo mara baada ya kiapo cha utii Ndugu Herbert Bilia ambae ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la Ilemela amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na tume huru ya taifa ya uchaguzi.
"Jambo kubwa ambalo ninawasisitiza washiriki wa mafunzo haya ni kuzingatia sheria taratibu kanuni na miongozo ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani na utulivu", amesema Ndugu Bilia

Sambamba na hilo Ndugu Bilia amewataka kujiepusha na kuwa vyanzo vya malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi, kufanya kazi kwa ushirikiano, kufika mapema kabla ya muda wa kufungua kituo kwa ajili ya maandalizi, kuwa nadhifu na kutumia lugha nzuri pamoja na kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalum pindi watakapofika kituoni.
Nao washiriki wa mafunzo haya wamesema kuwa wanatarajia kutokana na mafunzo watakayopatiwa wataenda kutekeleza jukumu lililopo mbele yao la kusimamia uchaguzi mkuu kwa huru na haki, kwa mujibu wa sheria sambamba na kuwa wazalendo huku wakiahidi kuviishi viapo vyao.
Jimbo la Ilemela lina jumla ya vituo 944 vya kupigia kura katika kata 19 na jumla ya watendaji wa vituo 3852 wakijumuisha wasimamizi wa vituo ,wasimamizi wasaidizi wa vituo, pamoja na makarani waongozaji wapiga kura 982.



Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.