Zaidi ya wasichana wasiopungua 2898 katika Manispaa ya Ilemela wanatarajia kunufaika na chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ambayo inaendelea kutolewa katika maadhimisho ya wiki ya chanjo ambayo huadhimishwa nchi nzima, bara na visiwani.
Akizindua rasmi chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na maadhimisho ya wiki ya chanjo kitaifa kwa Wilaya ya Ilemela, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Wanga ambae alimwakilisha mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe Khadija Nyembo, amesema kuwa lengo la maadhimisho ya wiki ya chanjo ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano ambao hawajakamilisha chanjo wanapata kwani chanjo ni haki ya kila mtoto.
Aidha alisema kuwa katika wiki hii ya chanjo, Wilaya ya Ilemela inatarajia kuchanja wasichana wasiopungua 2898 dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Katika wiki hii ya maadhimisho ya chanjo manispaa ya Ilemela tunatarajia kuchanja wasichana wasiopungua 2898 dhidi ya saratani ya mlago wa kizazi”, alisema
Aliongeza kuwa, sambamba na kutoa chanjo ya saratani, manispaa pia itatoa chanjo mpya ya kuzuia ugonjwa wa polio ambayo itatolewa kwa njia ya sindano na sio matone kama hapo awali.
Akihutubia wananchi, Mkurugenzi John alizitaja dalili za ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na kuzitaja sababu zinazochangia kuenea kwa ugonjwa huo ikiwemo kujamiiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi pamoja na uvutaji wa sigara huku shirika la afya ulimwenguni WHO likikadiria kuwa zaidi ya wagonjwa wapya 50,000 wa saratani ya mlango wa kizazi hubainika kila mwaka nchini Tanzania.
Nae kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela Bi Maria Kapinga amewatoa hofu wazazi juu ya chanjo hiyo ikiwa ni pamoja na kuwataka kuwaruhusu watoto wao kuhudhuria vituo vya kutolea huduma ili waweze kuchanjwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la afya (WHO) aliyehudhuria uzinduzi huo, Ndugu Arlen Galimo ameipongeza halmashauri kwa uzinduzi huo wa utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi amewaasa wahudumu wa afya wa manispaa hiyo kutimiza wajibu wao kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na magonjwa hayo.
Nchini Tanzania, maadhimisho ya wiki ya chanjo kwa watoto hufanyika kila mwaka wiki ya mwisho ya mwezi wa nne ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya katika Wilaya ya Ilemela yameambatana na uzinduzi wa chanjo mbili mpya ambazo ni chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na chanjo ya sindano ya kuzuia ugonjwa wa polio ikiwa na kauli mbiu ya ‘JAMII ILIYOPATA CHANJO NI JAMII YENYE AFYA, TIMIZA WAJIBU WAKO’
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.