Wasanii wa Ilemela wamesisitizwa kuandaa kazi zenye kuzingatia maadili, uzalendo, uelimishaji na ukosoaji kwa jamii katika kazi zao za sanaa wanazozifanya.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Dkt. Angeline Mabula wakati wa kikao chake na wasanii wanaofanya kazi zao za sanaa mbalimbali kama uigizaji,muziki,ngoma za asili,sarakasi na dansi ndani ya Wilaya ya Ilemela kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za CCM kata ya Buswelu.
Mhe.Mabula amefafanua kuwa kazi kubwa ya wasanii ni kuelimisha jamii dhidi ya mambo yasiyofaa tofauti na wasanii wengi wa nyakati hizi ambao wamekuwa wakiandaa kazi zisizoishi muda mrefu .
".. Sanaa mnayoifanya ina mafunzo gani katika jamii, zipo nyimbo za kina Baraka Mwinshehe na wengine zilikuwa zinatoa mafunzo ambayo mtu akisikiliza hata leo anayapata, Unaweza ukawa mchekeshaji lakini katika kuchekesha kuwe na ujumbe wenye maadili, unaweza kuwa mtunzi wa nyimbo lakini nyimbo unazoimba ziisaidie jamii .." Alisema
Aidha Dkt.Mabula amewaasa wasanii hao kuwa wamoja, kutambulika kisheria na kutumia fursa zilizopo za mikopo ya halmashauri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi sanjari na kujitokeza katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kujiandikisha katika daftari la mkazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Mwashum Ismail ni mwenyekiti wa chama cha wasanii wilaya ya Ilemela yeye amemshukuru mbunge huyo kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii hao pamoja na namna anavyoshiriki katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Akihitimisha kikao hicho diwani wa viti maalum kata ya Buswelu Bi.Winfrida Gyunda amewapongeza wasanii hao kwa kazi nzuri wanazozifanya katika jamii na kuwataka kuacha kulalamika na badala yake kutumia vipaji walivyonavyo kwa ubunifu zaidi kwa kushirikiana na serikali katika kujiletea maendeleo binafsi na jamii kwa ujumla.
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.