Kuelekea siku ya wanawake duniani Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia idara ya maendeleo ya jamii imeunganisha makundi mbalimbali ya wanawake wa Ilemela ikiwemo wadau kutoka mashirika ya siyo ya kiserikali, wafanyabiashara,wajasiriamali ,watumishi wa umma na wasio na shughuli rasmi katika tendo la kutoa kwa ajili ya wahitaji.
Wanawake hao walitembelea kata tatu za Kayenze ,Sangabuye na Bugogwa ambapo lengo kuu ilikuwa ni kuwatembelea watoto wanaoishi mazingira magumu ,watoto wanaojilea wenyewe ,watoto yatima na kutoa misaada ya hali na mali ikiwa ni sehemu ya kuwaonyesha upendo na kuwatia moyo kuishi bila kukataa tamaa na kutumia changamoto zao kama fursa.
“..Unaweza ukawa unapitia maisha magumu sana lakini hali hiyo isikusababishe kushindwa kusoma au kupoteza matumaini,wapo viongozi wengi wakuu wa nchi hii waliozaliwa na kukulia mazingira magumu sana.Tupo hapa kwa upendo msijisikie wanyonge ninyi ni watoto wetu..” Amesema Neema Majura Mratibu wa dawati la jenda Ilemela .
Sophia Nshushi ni mdau kutoka shirika lisilo la kiserikali la Teen Corridor Organization yeye anasema mtoto anapokuwa tumboni ni wa kwako akishazaliwa ni mtoto wa wote hivyo ushiriki wao katika matendo ya huruma kama hayo ni kawaida yao huku akiwasisitiza watoto wanaojilea wenyewe kuendelea kuwa na nguvu ya kupambana na vishawishi mbalimbali katika hatua zao za ukuaji kimwili na kihisia na kuhakikisha wanatimiza malengo waliojiwekea.
Zulfa Cornel (13) ni mwanafunzi kutoka shule ya msingi Bezi anatoa shukrani kwa kwa kina mama hao kwa misaada iliyotolewa huku akiahidi kusoma kwa bidii kutimiza ndoto zake za kuwa daktari.
Mwalimu Mashaka Edward Msiba ambae ni mlezi wa wanafunzi waishio kwenye mazingira magumu katika shule ya msingi Kisundi amewaombea kila lililo jema kina mama wote walioshiriki zoezi hilo la utoaji kwa wahitaji.
“..Mungu awabariki sana kina mama kwa kijitoa kwenu ,mmetoa muda wenu, pesa zenu kwa ajili ya hawa watoto.Mungu awazidishie pale mlipotoa..”
Jumla ya watoto 60 wamenufaika na msaada huo ambapo vitu vilivyotolewa ni mchele,sukari,mafuta ya kupikia,sabuni za unga ,sabuni vipande na za maji,mafuta ya kupaka ,dawa za meno na mahitaji madogo madogo ya shule kama madaftari na kalamu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.