Na Paschalia George
Wanafunzi wa shule za sekondari katika Manispaa ya Ilemela wamejengewa uwezo wa kutambua na kuripoti vitendo vya unyanyasaji, ukatili,uvutaji bangi na madawa ya kulevya na kujiepusha na mimba katika umri mdogo ili kujenga taifa lililo bora lenye wataalam wenye weledi na mlengo chanya kimaendeleo
Akizindua mpango huo wa kutoa elimu ya kujitambua na kupambana na vitendo vya ukatili mashuleni, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa ni wajibu wa jamii nzima ya Ilemela kila mmoja kwa nafasi yake kuelimisha wanafunzi juu ya mambo mbalilmbali yanayowahusu katika makuzi yao sambamba na kutoa pongezi kwa uongozi wa jeshi la polisi na Halmshauri ya manispaa ya Ilemela kwa kuungana katika kubuni jambo hili lenye manufaa kwa wanafunzi na jamii nzima ya Ilemela.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Dkt Mabula ametoa rai kwa wanafunzi kujiepusha na matukio yote yasio na faida kwao huku akisisitiza wanafunzi hao kujiepusha na uvutaji bangi na matumizi ya madawa ya kulevya,mimba mashuleni ,vitendo vya unyanyasaji na ukatili.
“Wanangu wa kike nataka mjiepushe na lifti hasahasa za bodaboda, msipende vya bure. Kila mmoja afahamu kwa nini yuko hapa,wazazi wamewaleta shuleni msome jukumu lenu kubwa ni hilo. Muwe wepesi kutoa taarifa za matukio yasiyo ya kawaida punde yanapojitokeza”
Nae Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Wilaya ya Ilemela Afande Shamira Kasimu Mkomwa amezungumzia kwa undani juu ya madhara ya madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na mtumiaji kutengwa na jamii kwa sababu ya kuwa na mambo ya hovyo hovyo yasiyo na tija sambamba na madhara ya kiuchumi ambayo yanasababisha jamii kuwa duni katika masuala ya kimaendeleo.
“ Hatuitaji taifa lenye wataalam wavuta bangi wala madawa ya kulevya, wanyanyasaji au viongozi wenye matukio ya ajabu ajabu yasiyofaa kwa maadili yetu ya kitanzania tunataka taifa lenye uhai na watu timamu. Mtoe taarifa haraka kwa jeshi la polisi punde mnapoona moja ya matukio hayo kwani jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao.”amesema
Wanafunzi hao pia wamenufaika na elimu ya usalama barabarani iliyotolewa na kaimu afisa usalama barabarani wilaya ya Ilemela afande Hosiana Mushi kwa kuwasisitiza juu ya umakini na kufuata sheria pindi wanapotumia barabara.
Aidha Afisa elimu sekondari ndugu Emmanuel Malima amewaasa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani ndilo jambo pekee litakaloonyesha nuru katika maisha yao.
“Wasichana chipsi ni chakula cha kawaida tu msitoe utu wenu kwa ajili ya chipsi,wavulana pia achaneni na magenge yasiyofaa kuja shule kukaa kwenye mawe au maporini amkeni wanangu muone umuhimu wa nyie kuwepo hapa”amesema
Mwanafunzi, Joseph Elias Masanja ameshukuru kwa elimu iliyotolewa kwani itawasaidia katika kubaini na kuripoti matukio yote yasiyofaa katika jamii tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa ngumu kwao kubaini aina za matukio ya ukatili na hatua za kuchukua.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.