Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza wametakiwa kuzingatia mpango kabambe (master plan) wa matumizi ya ardhi ili kuepuka ujenzi holela na kushusha thamani ya ardhi wanazomiliki .
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe. Dkt. Angeline Mabula wakati wa zoezi la kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero na changamoto za ardhi kupitia kliniki ya ardhi iliyofanyika katika ukumbi wa Winterfell kata ya Nyasaka ambapo amefafanua kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kuandaa mpango huo kabambe wa matumizi ya ardhi unaolenga kutoa muongozo wa namna bora ya kupanga mji kulingana na matumizi yake .
“.. Mkoa wetu wa Mwanza kwa bahati nzuri unao mpango kabambe wa matumizi ya ardhi, mpango ambao umefafanua kila eneo limepangwa kwa matumizi gani, unakuta mtu eneo zima amejenga fremu tu na jirani yake fremu utafikiri hakuna uwekezaji mwengine.Tukiufuata mpango kabambe umeelekeza wazi wapi tunapaswa kufanya nini na kama hauwezi basi muingie mikataba na wawekezaji wengine ili kuongezea thamani maeneo yetu ..” Alisema
Aidha Mhe. Dkt. Mabula amezitaka mamlaka za ardhi mkoa wa Mwanza na manispaa ya Ilemela kuzingatia maelekezo ya kamati ya bunge juu ya kurejesha eneo la shule ya sekondari Kisenga kata ya Kiseke na kumlipa fidia mwananchi aliyetwaliwa eneo lake au kumpatia eneo jingine ili shule hiyo iweze kuwa na eneo la kutosha kukidhi mahitaji yake na kutekeleza maelekezo ya kamati hiyo.
Kwa upande wake kamishina wa ardhi msaidizi mkoa wa Mwanza Bi. Happines Mtutwa amesema jumla ya hati miliki 95 za maeneo tofauti ndani ya Manispaa ya Ilemela zimetolewa kwa wananchi huku akipongeza zoezi la kliniki ya ardhi linaloendelea kuwa limekuwa la mafanikio makubwa kwa kupunguza kero nyingi za ardhi Ilemela.
“..tumetumia mbinu za kuweka kambi maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi kusikiliza na kutatua kero zao za ardhi huku tukiwaelimisha juu ulipaji kodi za ardhi na elimu ya master plan ili wajue mgawanyo wa matumizi ya ardhi ..”
Nae diwani wa kata ya Nyasaka Mhe. Abdulrahman Simba amempongeza mbunge huyo kwa kazi nzuri anayoifanya ndani ya jimbo lake.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.