Ikiwa ni siku ya saba (7) toka kuanza kwa kliniki ya ardhi ndani ya Manispaa ya Ilemela, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Wakili Mariam Msengi, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amekabidhi hati 100 kati ya hati 376 ambazo zimekwishaandaliwa kwa wanachi wanaomiliki ardhi ndani ya Manispaa ya Ilemela.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hati hizo, Wakili Mariam amewataka wananchi kutumia fursa hii ya kliniki ya ardhi kwa ajili ya utatuzi wa changamoto yoyote ile ya ardhi inayopelekea kushindwa kupata hati sambamba na kuwataka kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi wanaopitia changamoto za ardhi kwani mahali hapa ni salama na sahihi kwao.
“Zoezi hili ni kutokana na maelekezo ya Mhe Rais, ambapo alielekeza kusogeza huduma kwa wananchi wetu, na huduma imesogezwa clinic hii itakuwa ni endelevu hivyo mwenye changamoto yoyote ile ya ardhi ikihusisha kupata hati, migogoro katika maeneo yetu ambayo inapelekea kushindwa kupata hati hapa ni eneo sahihi” Alisema Wakili Mariam
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kliniki hiyo Afisa ardhi mteule wa Manispaa ya Ilemela Bi.Grace Masawe amesema zaidi ya hatimiliki 376 zimeandaliwa na kusajiliwa, migogoro 93 imepokelewa huku migogoro 23 katika hiyo ikipatiwa ufumbuzi wa kudumu na migogoro mingine ikiwa ipo katika hatua mbalimbali za kutatuliwa, ambapo wananchi 211 wamesikilizwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya ardhi.
Nae kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza Bi.Happiness Mtutwa amewataka wananchi kufika ofisi za ardhi na kupata huduma wanazohitaji kwani wapo tayari kuwahudumia na kuwaondolea kero zinazowakabili.
“Tuna utayari na tupo tayari kuwahudumia wananchi na tunatamani asiwepo mwananchi wa Manispaa ya Ilemela /Mkoa wa mwanza anaelalamika kuhusiana na kutopewa huduma zetu ipasavyo au kutopata hati kwa wakati”.Alisema Bi Mtutwa
" Serikali ya awamu ya sita ipo kazini kutatua kero na shida za wananchi iwapo mwananchi umehudumiwa na hujaridhika fika ofisini na iwapo unazungushwa toa taarifa utapata haki yako,Ni matamanio yangu, zoezi hili la kliniki ya ardhi lifanyike kila robo mwaka ndani ya Manispaa yetu ili tuweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutatua kero nyingi kwa muda mfupi." Amesema Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Adv.Kiomoni Kibamba.
Wananchi ambao wamefika kwa ajili ya kupata hati wamefurwahishwa na zoezi hili huku wakiishukuru Serikali na kusema kuwa limewarahishia kupata hati ndani ya muda mchache tofauti na ilivyokuwa hapo awali.Huku wakiwataka wananchi wenzao kuacha kukaa na kero na kuanza kufuatilia migogoro hiyo
“Kuanzia sasa hivi hati zitatoka, wenye migogoro itakwisha tusikae nyumbani kwa kuwaza kuwa ukifika utapigwa tarehe sasa hivi hamna cha tarehe mambo yako wazi kabisa wananchi tuamke nimefurahi sana kupata hati” Amesema Bi Priscila Desderi Mato mkazi wa Nyambiti Buzuruga
Elizabeth Magiri ni mkazi wa kata ya Nyasaka yeye anashukuru uongozi wa Ilemela kwa kuandaa huduma hiyo iliyomuwezesha kupata hati yake kwa muda mfupi kwani ni ulinzi wa kudumu wa ardhi yake
“Nilipigiwa simu kuja kuchukua hati ya kiwanja kilichopo Ilemela, ikiwa ni muda mfupi baada ya kufanya malipo na nikaambiwa kuichukua kwa kamishna tarehe 24 lakini nashangaa kabla ya tarehe 24 nimeipata hati yangu” Alisema Paul Bruno ambae ametokea Wilaya ya Ukerewe kata ya Bukindo,
Zoezi hili la kliniki ya ardhi litahitimishwa siku ya Ijumaa tarehe 19 Januari 2024, hivyo wananchi wametakiwa kuwasilisha nyaraka zao kwa ajili ya kuandaliwa hati miliki sambamba na kufika ofisi za Manispaa kuchukua hati zao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.