WANANCHI WATAKIWA KUTOJENGA KWENYE KINGO ZA MITO
Kamati ya Ardhi na Mipangomiji ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imewataka wananchi wake kuacha ujenzi wa nyumba pamoja na uendeshaji wa shughuli za kibinaadamu katika maeneo ya kingo za mito.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa kamati ya mipango miji ya manispaa Mheshimiwa Alex Ngusa ambaye pia ni diwani wa kata ya Kirumba wakati wa ziara ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika kipindi cha robo ya tatu iliyojumuisha matengenezo ya sehemu korofi za barabara ya Nyafula-Igumamoyo yenye urefu wa kilomita 2.5, ukaguzi wa eneo la mradi wa mji wa makazi(Nyafula Satellite), mradi wa maji Sangabuye, mradi wa maji Igombe, matengenezo ya muda maalumu ya barabara ya Mihama yenye kilomita moja, ukaguzi wa kingo za mto Vijana Social wa Kirumba-Nyamanoro na daraja la Msumbiji.
Mheshimiwa Alex Ngusa ambae ndie Mwenyekiti wa kamati hiyo amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za ardhi na ujenzi kwa kuacha kujenga nyumba kwenye kingo za mito sambamba na kujishughulisha na shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hayo.
“Dhamira yetu si kuwakosesha wananchi makazi shida ni wananchi kujenga maeneo ya kingo za mito tuwaombe waache kufanya hivyo kwani kunasababisha uharibifu wa miundombinu ya serikali kama hii barabara hapa na baadae watailaumu Serikali”, alisema.
Pamoja na hayo amewataka watendaji wa kata na mitaa kushirikiana na viongozi wa maeneo yao katika kupambana na vitendo vya uchimbaji mchanga katika maeneo yote kingo za mito hiyo ili kupambana na uharibifu wa mazingira.
Nae afisa mipango miji wa manispaa hiyo ndugu Kennedy Chigulu amesema kuwa kwa kufuata ramani za miaka ya nyuma eneo hilo linaonesha kuwa wazi tofauti na sasa ambapo eneo linaonesha kuvamiwa na wananchi kinyume na taratibu wa mipango miji
“Ukitazama ramani za miaka ya sabini zinaonesha kuna wananchi wamevamia maeneo ya kingo za mito, Tukiacha kufanya shughuli za kibinadamu maeneo ya mito athari hazitakuwepo kwa jamii”, Alisema.
Wakihitimisha Ziara hiyo, wajumbe wa kamati ya ardhi na mipangomiji wameiagiza idara ya mipango miji kukaa pamoja na viongozi wa maeneo ya mto Vijana Social Kirumba-Nyamanoro ili kupitia upya ramani za eneo hilo ili kuweza kudhibiti ujenzi holela wa makazi na uendeshaji wa shughuli za kibinadamu katika kingo za mto huo pamoja na kuchukua hatua za haraka kunusuru usambaaji hovyo wa maji katika kipindi cha mvua kubwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.