Wananchi wa wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kukitunza na kukitumia vizuri kivuko cha MV Ilemela ili kiweze kudumu kwa muda mrefu na kuwakomboa kiuchumi.
Hayo yamesemwa na mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa uzinduzi wa kivuko hicho katika eneo la mwalo wa Kayenze wilayani humo ambapo amewataka wananchi hao kuhakikisha wanakilinda kivuko hicho, wanakitunza na wanakitumia vizuri kwa shughuli za uzalishaji mali ili kiweze kuleta manufaa kwa jamii na kuwainua kiuchumi badala ya kufanya uharibufu wa aina yoyote na kuiba vifaa vilivyomo ndani ya kivuko hicho.
‘.. Ndugu zangu tukitunze kivuko chetu, hii ni mali yetu, tukianza kuhujumu basi tujue tunajihujumu sisi wenyewe, lazima kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie katika kuhakikisha kivuko hichi hakiharibiki ...’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula alimshukuru Mhe Rais Dkt John Magufuli kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha adha ya usafiri iliyokuwa ikiwakabiri wananchi wa kata ya Kayenze na kutoa fedha za ujenzi wa kivuko hicho, Sanjari na kuwataka wananchi wa Kayenze kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Korona huku akiomba wataalamu wa afya kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo ndani ya Kivuko kabla ya kuanza kwa safari na mwisho wa safari.
Kwa upande wake mkurugenzi wa wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle amesema kuwa kivuko hicho kitaanza safari zake rasmi kuanzia Aprili 19, 2020 ambapo wananchi watasafiri bure na baadae kuanzia Aprili 20, 2020 kila mwananchi atalazimika kulipa nauli ya shilingi elfu moja kwa kila safari atakayoifanya huku gharama za mizigo ikitegemea ukubwa na uzito wa mzigo wenyewe.
Nae mkazi wa Bezi Peter Masalu ameshukuru kwa kuzinduliwa kwa safari ya kwanza ya kivuko hicho na kuahidi kukitumia kivuko hicho kwa kujiongezea kipato kupitia biashara ya usafirishaji samaki.
Akihitimisha mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Nelson Mesha amempongeza Rais Dkt Magufuli na mbunge wa Ilemela kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM na kuwaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu tano katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.