Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu hasa kwa wanaoishi maeneo ya kando mwa ziwa viktoria kwa kuzingatia usafi na kula vyakula vya moto na salama
Rai hiyo ameitoa wakati wa muendelezo wa ziara ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi aliyoifanya katika viwanja vya ofisi ya kata ya Kawekamo ambapo amesema kuwa Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo lakini juhudi hizo haziwezi kuzaa matunda kama wananchi wataendelea kutozingatia usafi na kuendelea kula ovyo
‘.. Nawakumbusha wananchi wetu kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu, Tuna watu kama 100 hivi wameshapita katika kituo chetu cha magonjwa ya mlipuko pale Buswelu, Lakini tatizo kubwa lipo kule Bugogwa nako tumeshapokea wagonjwa 100 hivi, Ugonjwa huu shida yake kubwa ni uchafu ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala amewaagiza watendaji wa mitaa na kata kusimamia usafi katika maeneo yao pamoja na kuwataka mawakala wa usafi kuongeza kasi katika ukusanyaji wa taka katika maeneo yao tofauti na utaratibu waliojiwekea wa kukusanya siku chache katika wiki
Nae Daktari Michael Kiremeji kutoka wizara ya afya amesema kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu yanahitaji nguvu ya pamoja kwa wananchi kushirikiana na Serikali na si kuiachia Serikali peke yake au kikundi cha watu wachache kwa kuwa ugonjwa huo ni wa aibu
Valentine Sanga ni mtaalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha majanga amefafanua kuwa hata kama wataalam wa nchi nzima wataweka kambi wilaya ya Ilemela kama wananchi wenyewe hawatachukua hatua dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo basi itakuwa kazi bure na madhara yatazidi kujitokeza
Bi Sophia Selemani mkazi wa Kawekamo mbali na kuipongeza serikali kwa kutoa elimu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo amesema kuwa yeye binafsi amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha anazingatia usafi wa mazingira yanayomzunguka nyumbani kwake na kula vyakula visafi na salama huku akiwashauri wananchi wenzake kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa afya .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.