Wananchi wa mtaa wa Lukobe katika kata ya Kahama iliyopo Manispaa ya Ilemela wanatarajia kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya afya mara baada ya ujenzi wa zahanati ya Lukobe kukamilika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Mtaa Lukobe Ndugu Paulo Lameck amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huu, wananchi wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma ya afya.
“Wananchi wa lukobe wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu wa takribani Kilomita 10 hadi 20 kwa ajili ya kutafuta huduma za afya”, Alisema ndugu Paulo
Nae Mtendaji wa Mtaa wa Lukobe Ndugu Egno Mayaka amesema kuwa, ujenzi wa zahanati uliibuliwa na wananchi wenyewe mara baada ya kuona wanapata tabu ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma ya afya mtaani hapo kwa kujenga msingi kwa kutumia nguvu zao ambao hadi kukamilika kwa msingi iliwagharimu kiasi cha Shilingi Milioni 7.4 za kitanzania.
Mtendaji wa Kata ameongeza kwa kusema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo unafanyika kwa ushirikiano wa mfadhili kutoka Canada Ndugu Dawn Schaller ambae ni rafiki wa karibu wa mtaa huo , ambae amejenga boma la zahanati hiyo pamoja na kupiga plasta ambapo ujenzi huo hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 15.6 za kitanzania, na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela nayo imechangia zoezi la upauaji wa zahanati hiyo na hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 13 za kitanzania.
Nae Mbunge wa Ilemela Mhe. Dr. Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa zahanati hiyo amewashukuru wananchi na wadau wa maendeleo waliofadhili ujenzi wa zahanati hiyo na kuahidi kuvuta maji pamoja na kuongeza matofali kwa ajili ya ujenzi wa choo cha karibu na zahanati.
Hadi sasa ujenzi huu ambao umefikia hatua ya upauaji unatarajiwa kukamilika mwaka 2019, na hadi sasa gharama zilizotumika ni jumla ya fedha za kitanzania Shilingi Mil.36 ikiwa ni mchango wa Halmashauri, mfadhili na wananchi wa mtaa wa Lukobe.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.