WANANCHI WA ILEMELA WATAKIWA KUTII SHERIA BILA SHURUTI
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga amewataka wananchi kutii sheria bila shuruti kwa kufuata taratibu ili kuweza kuyafikia malengo ya serikali katika kuwaletea maendeleo.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Shibula juu ya utatuzi wa mgogoro wa ardhi unaohusisha eneo la jeshi la wananchi kikosi cha anga, eneo la uwanja wa ndege na wananchi hao ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makaazi Daktari Angeline Mabula alilolitoa mapema wiki hii baada ya kufanya kikao na wananchi hao.
“Siku hizi kumekuwepo na vizazi visivyofuata haki na wajibu na hiki ndicho kinachofanya sheria zivunjwe, Niwaombe sana unapodai haki ni lazima utimize wajibu wako tusiwe kama wale watu wanaotumwa na wazungu kusababisha vurugu ili waweze kulipwa pesa, Nawaomba tena ndugu zangu tufate sheria na taratibu, Tusikubali kutumika na viongozi wachache wenye maslahi yao binafsi kwa kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani pasipo sababu ya msingi”, Alisema.
Aidha Mkurugenzi Wanga amewataka viongozi wa maeneo yanayoguswa na mgogoro huo kuacha mara moja kushawishi wananchi kugomea utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kushinikiza vitendo vya kihalifu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote kwa ridhaa yake ama kushawishiwa atakaejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani huku akiwaasa juu ya kudai haki zao kwa utaratibu unaokubali na usioleta madhara kwa wengine .
Kwa upande wake afisa mipango miji wa Manispaa ya Ilemela Anna Mhamba amewahakikishia wananchi hao kuwa siku ya jumatatu atashirikiana na wataalamu wengine kufika eneo la tukio kubaini mipaka inayolalamikiwa na pande zote na mwisho kuwasilisha taarifa hiyo kwa ngazi husika ili iweze kufanya maamuzi sahihi yenye maslahi mapana kwa pande zote yakizingatia haki bila uonevu kwa yeyote.
Nae Diwani wa kata ya Shibula Mheshimiwa Swila Dede kwa niaba ya wananchi ameushukuru Uongozi wa Ilemela kwa namna inavyolishughulikia suala hilo huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo la utatuzi wa suluhu ya mipaka ya pande hizo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.