Wananchi wa manispaa ya Ilemela wametakiwa kupanda miti kwa wingi itakayosaidia kutunza mazingira ili kwenda sambamba na mpango wa Serikali wa upandaji wa miti kuzuia athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Rai hiyo imetolewa leo na diwani wa kata ya Buswelu mheshimiwa Sarah Ng’wani wakati wa zoezi la upandaji miti liliendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la MWAOMI lililo chini ya kanisa la FPCT Ilemela katika viwanja vya Zahanati ya Nyerere ambapo zaidi ya miti 5000 imekusudiwa kupandwa katika maeneo tofauti tofauti ya manispaa hiyo huku miti 2000 ikipandwa mpaka sasa kwaajili ya kutunza mazingira ambapo amewaasa watendaji wa serikali na wananchi kuhakikisha wanapanda miti, wanaitunza na kuilinda ili kuwa na mazingira yaliyo salama.
Aidha amewataka watendaji wa serikali kuhakikisha wanakamata wananchi wote wanaovunja sheria za mazingira na kusababisha uharibifu kwa kuchunga mifugo maeneo ya miji yasiyoruhusiwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa nyuki wa manispaa hiyo Bi Perpetua Moyo amesema kuwa bado ipo changamoto ya upatikanaji wa miti, uelewa juu ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira hivyo ameishukuru taasisi hiyo kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo sanjari na kuwaomba viongozi wa mitaa kutunza miti iliyokwisha pandwa katika maeneo yao.
Nae mratibu wa shirika la MWAOMI Bwana Fredrick Eliackim Rubinde amesema kuwa shirika lake limekuwa likiendesha kampeni tofauti tofauti kwa manufaa ya jamii, kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa hapo jana katika viwanja vya shule ya sekondari Bujingwa ni miongoni mwake huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo ni endelevu, Pamoja na kutaja faida mbalimbali za miti kwa Umma ikiwemo uzalishaji wa hewa safi, uzalishaji wa mbao, uzalishaji wa dawa, kuchochea mvua, kutunza maji na chakula.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.