Serikali kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF), inalenga kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa na kulinda maslahi ya watoto wao, kwa kuhakikisha watoto wenye umri wa kupelekwa kliniki wanapelekwa na wanafunzi wanapatiwa mahitaji ya shule
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni miongoni mwa halmashauri ambazo zimeendelea kunufaika na mpango huu wa kunusuru kaya maskini kwa kupokea fedha ambazo hutolewa kwa walengwa wa kaya maskini pia kwa ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Katika kipindi cha robo ya kwanza Julai hadi Septemba mwaka wa fedha 2024/2025, Manispaa ya Ilemela imepokea jumla ya fedha kiasi cha shilingi milioni 800.86 (Tshs 800,864,599), ikiwa ni fedha kwa ajili ya walengwa wa kaya maskini na fedha kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za kijamii
Kati ya fedha hizo shilingi milioni 216.07 (Tshs. 216,076,310) ni fedha kwa ajili ya malipo ya walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini kwa kaya 3447 zinazonufaika na mpango huo.
Kwa upande wa uboreshaji huduma za kijamii na kiuchumi shilingi milioni 584.78 (Tshs 584, 788,289.97) zimepokelewa katika robo ya kwanza 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata za Kayenze na Kiseke. Kwa upande wa kata ya Kiseke shilingi milioni 101.23 zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na shilingi milioni 483.55 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya na elimu katika kata ya kayenze.
Sikujua Maluba Migisi ni mnufaika wa mpango huu wa kunusuru kaya maskini kutoka mtaa wa Butuja kata ya Ilemela, yeye anaishukuru TASAF kwani kupitia mpango huu ameweza kuwanunulia Watoto wake mahitaji ya shule lakini si hivyo tu fedha hiyo imemuwezesha kufungua biashara ndogo ambapo faida ikipatikana humsaidia kukidhi mahitaji ya nyumbani na watoto shuleni huku akiwakumbusha wakina mama wenzake kuwa wanapopata fedha hizi wazitumie kwenye biashara kukuza mtaji wao na matumizi ya nyumbani.
Bwana Sinja Jumanne mkazi wa mtaa wa PPF kata ya Kiseke, anasema kuwa kabla ya kujiunga na mpango wa TASAF Maisha yake yalikuwa chini sana lakini sasa maisha yameboreka kwani kupitia fedha hizo ameweza kukodi mashamba ambapo kupitia kilimo anapata kipato cha kukidhi mahitaji yake na ya familia yake.
Betia Nyajoro mkazi wa mtaa wa Isenga kata ya Kiseke anasema awali alikuwa anaweza kukosa hata fedha ya kununua mahitaji ya shule ya Watoto wake, lakini kupitia fedha hiyo ya TASAF alianzisha biashara ndogo ambapo hadi sasa mtaji wake umeenda unakua, amewashari wanufaika wenzake kuwa pindi wapatapo fedha hii wasiendekeze pombe bali watumie fedha hizo kuanzisha biashara ndogo ndogo ili kukuza kipato chao
“Fedha hii ukiitumia kwa malengo inakuinua, tusiidharau kuwa ni fedha ndogo inatusaidia sasa hivi hali niliyo nayo mimi sio kama awali kabla sijajiunga na mpango huu wa TASAF” alisema Bi Betia.
Nao wananchi wa mtaa wa Bezi kata ya Kayenze katika nyakati tofauti wameishukuru serikali kwani kupitia fedha za TASAF sasa kisiwa cha Bezi kinaenda kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kiasi cha shilingi milioni 202.46 zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje na ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa afya.
Leonard Robert ni mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela, ametoa rai kwa walengwa wa mpango huu kwa kuwataka walengwa hao kujiunga kwenye vikundi vya walengwa ili kujijengea utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza ili watakapohitimu katika mpango waweze kujitegemea kiuchumi.
Mwisho amewataka walengwa hao kutumia ruzuku wanazopokea katika kuanzisha au kuendeleza biashara ndogondogo, ufugaji, kuboresha makazi ,kilimo cha bustani na kuhudumia familia zao.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.