Wananchi wa Wilaya ya Ilemela wametakiwa kuhakikisha kuwa usafi unakuwa ni agenda ya kudumu ya kila siku kwani usafi ni kwa ajili yetu sote.
“Nitoe rai yangu kwenu kuwa zoezi la usafi liwe agenda ya kudumu ya kila siku kwani usafi ni kwa ajili yetu sote tuliendelea kufanya usafi tutaweka mji wetu salama na kuepukana na magonjwa”Alisema Mariam Msengi Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela.
Bi Mariam Msengi ameyasema hayo akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika KILELE CHA maadhimisho ya siku ya usafi Duniani ambayo hufanyika tarehe 16 Septemba ya kila mwaka ambapo katika Manispaa ya Ilemela maadhimisho hayo yalifanyika kwa kufanya usafi katika soko la magomeni Kirumba.
Peter Joseph ambae ni Afisa Usafishaji na Mazingira wa Manispaa ya Ilemela alisema kuwa zoezi la usafi ni ajenda ya kudumu katika maeneo yote ya kufanyia biashara na kazi , kwani usafi sio kitu cha siku moja ni jambo la kila siku na kuongeza kusema kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanatokana na uchafu hivyo endapo mtu ataweza kudhibiti uchafu ataepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu.
“Tumeanza na maeneo ya masoko kwa sababu tunaamini ni sehemu kubwa ya uzalishaji wa taka ngumu hivyo taka ngumu zinatakiwa zidhibitiwe ili zisiwe chanzo cha mlipuko wa magonjwa kwasababu sehemu kubwa ya wanajamii wanapata huduma masokoni endapo patakuwa pachafu wataondoka na maradhi kutoka eneo la soko na kupeleka kwa wanajamii wanapoishi” alisema Ndugu Peter
Mwenyekiti wa soko la Magomeni Ndugu Elias Daud alitoa rai kwa wafanyabiashara kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi ambao walikuwa nao awali na kwa wafanyabiashara ambao wana maeneo ndani ya soko na wameenda kuuzia nje amewataka kurudi ndani ya soko ili waweze kuepusha mlundikano wa taka ndani ya soko kufuatia kwamba wafanyabiashara wamekuwa wakitumia vibanda ambavyo havina watu kutupia taka.
Nae Mhudumu ngazi ya jamii kutoka kata ya Kirumba ameomba zoezi hili kuwa ni endelevu kwani hali ya usafi sio nzuri, lakini utaratibu huu ukiendelea basi usafi wa mji utaimarika, alisema.
Kilele cha siku ya usafishaji duniani kwa mwaka 2023 kilienda sambamba na kauli mbiu isemayo “Tuungane pamoja kujifunza kupanga na kuhimiza uimarishaji huduma za udhibiti taka”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.