Wananchi kutoka kata mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wameitikia wito wa kampeni ya ujenzi wa madarasa inayoendelea katika Manispaaa hii, hilo limedhihirishwa baada ya wananchi hao kujitokeza katika zoezi la uchimbaji wa msingi kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Msingi mpya katika kata za Kahama, Shibula na Buswelu ambalo linaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hasan Masala.
Wananchi hao wamesema wamelazimika kujitokeza katika zoezi hili la uchimbaji msingi kwa ajili ya uanzishwaji wa shule za msingi mpya katika kata hizo kufuatia changamoto mbalimbali ambazo watoto wao wamekuwa wakizipata.
Wakizitaja changamoto hizo kwa nyakati tofauti wamesema kuwa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufika shuleni, msongamano wa wanafunzi katika madarasa, walimu kuwa na mazingira magumu ya, walimu kushindwa kufuatilia wanafunzi vizuri darasani ni baadhi ya changamoto zilizopelekea wananchi wa Ilemela kuitikia wito wa kushiriki kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata mbalimbali.
"Ujenzi wa shule hizi mpya utawawezesha walimu kuwafuatilia wanafunzi darasani kwa ukaribu kutokana na kuondokana na msongamano wa wanafunzi, itaondoa utoro shuleni, utaongeza ufanisi katika ufundishaji pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia pamoja na kuboresha taaluma katika kata hizo". walisema
Nae Mwalimu Rehema Suleyman wa kata ya Kahama amewataka wanajamii kujitokeza katika mazoezi haya kwani ni faida ya watoto wao na kuonyesha kuwa ipo shida na uhitaji wa miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja kutoa moyo kwa serikali inayopambana kila siku ambayo inahakikisha inapatikana miundombinu katika sekta ya elimu
Akishiriki zoezi la uchimbaji wa misingi katika kata hizo, Mhe. Hasan Masala Mkuu wa Wilaya ya Ilemela akiwa na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi na wataalam wa Manispaa ya Ilemela, amebainisha malengo ya zoezi hilo ni kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya uhaba ya vyumba vya madarasa katika wilaya ya Ilemela hali inayopelekea wanafunzi kukosa maeneo ya kujifunzia.
“Kiwilaya tuna upungufu wa vyumba vya madarasa takriban 1200, hivyo tumeonelea ni lazima sisi wenyewe tupambane kuhakikisha tunapunguza uhaba wa vyumba vya madarasa na ikiwezekana tunaondoa kabisa changamoto hii”, amesema Masala
Aliongeza kwa kuiomba jamii kutoa ushirikiano wa kutosha huku akiwasisitiza kuwa wajenge maboma na Halmashauri itamalizia kwa kuezeka, na kuweka madawati katika shule hizo mpya huku akiwapongeza kwa utayari wao.
Mhandisi Modest Apolinary Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amewapongeza wananchi kwa jitihada zao za kushiriki ujenzi wa miradi ya maendeleo,na kuwaahidi kuwa mara baada ya maboma hayo kukamilika halmashauri itawajibika na suala zima la kukamilisha majengo hayo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.