Wananchi wa Manispaa ya Ilemela wameendelea kunufaika na mpango wa taifa wa kunusuru kaya maskini awamu ya tatu (TASAF III) kipindi cha pili, ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi Milioni 107,112,000 zimelipwa kwa walengwa 2262 walio katika mpango huo katika mitaa 100 ya Ilemela.
Akizungumza na walengwa wa TASAF wa kata ya Buswelu wakati wa utoaji wa mafunzo ya matumizi bora ya pesa hizo, mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh amesema kuwa ni wajibu wa kila mlengwa kutumia pesa zake vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Ni utaratibu wetu kila mara tunapotoa pesa hizi kutoa elimu kwa walengwa kubuni miradi midogomidogo itakayokuwa chachu ya kukuza vipato vyao kwa kasi ndogo lakini miradi itoe matokeo na kuonyesha ukuaji wao katika kujinasua na hali duni ya kiuchumi”, Alisema
Aidha alisema kuwa TASAF III imetambua changamoto za upokeaji pesa mkononi ikiwa ni pamoja na kufanya matumizi nje ya mpango wakati walengwa wanaporudi majumbani hivyo kuanzisha utaratibu wa kulipa pesa kwa njia ya benki badala ya kupewa pesa mkononi.
Halikadhalika alisisitiza matumizi bora ya pesa hizi kwa kujiunga na utaratibu wa mfuko uliopo sasa wa kufanya malipo kwa njia ya mtandao kupitia simu ,mawakala na benki kwani njia hii ni salama zaidi kwa vile inampa fursa mtumiaji kupanga na kuamua kwa utulivu zaidi kabla ya kushika pesa.
Kwa upande wake Sophia William Shabushi (70) wa mtaa wa Ibaya kata ya Shibula ambae ni miongoni wa walengwa ameishukuru serikali kwa mpango huu, kwani umempa pesa angalau kuweza kuanzisha miradi midogo midogo ya kumuwezesha kujikimu kiuchumi.
“Sasa hivi nina kibanda cha kuuza mbogamboga na matunda pale nyumbani ninapoishi,kwa siku sikosi elfu mbili kiasi kinachoniwezesha kumudu mahitaji madogomadogo kwangu na wajukuu zangu ikiwa ni pamoja na chakula .Nashukuru sana mpango wa TASAF kwani kweli ni mkombozi wetu” alisema
Hadi sasa Wilaya ya Ilemela imefanikiwa kusajiri kaya 1081 zinazoendelea kupata huduma za kifedha mtandaoni na zoezi la usajili likiwa bado linaendelea.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.